ZITTO KABWE ASIMULIA MAZITO BAADA YA KUKUTANA NA TUNDU LISSU

Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe amefunguka na kudai amerudi nchini akiwa na unyenyekevu mkubwa zaidi kwa sababu ya nguvu na ujasiri alioonyeshwa na Mbunge Tundu Lissu pindi alipokwenda kumjulia hali katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya.


Zitto ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa facebook asubuhi ya leo na kusema japo Lissu ameumizwa sana lakini hakuacha kumuonyesha ucheshi licha ya kuwa na maumivu makali aliyokuwa nayo katika mwili wake.


"Siku mbili hizi nilizoenda kumuona Lissu zimeniacha nikiwa mawazo sana, nimerudi nchini nikiwa kwenye unyenyekevu zaidi kwa sababu ya nguvu na ujasiri ambao ndugu yangu amenionesha licha ya kuwa kwenye maumivu makali. Siyo mara nyingi hapa nchini kusikia tukiongelea ujasiri lakini namfikiria lissu na vile nilivyojisikia nikiwa pamoja naye Nairobi, najua hivyo ndivyo alivyo", ameandika Zitto.


Pamoja na hayo, Zitto ameendelea kwa kusema "waliomshambulia wamemuumiza kweli na bado wakati tuliokuwa naye amenionesha shukrani, ari na pia ucheshi. Huo ni ujasiri, alichopitia na anachoendelea kupitia Lissu siyo kitu rahisi kwa mtu yeyote kutafakari. Kufikiria hali ile kungeniacha niumie moyo kama asingesema maneno haya kwangu kuwa 'tumeshinda. Tumeshashinda", amesisitiza Zitto.


Mbunge Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma na baadaye kusafirishwa kwenda jijini Nairobi Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu kufuatia majeraha aliyopata, ambapo mpaka sasa yuko huko kwa matibabu.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527