Na William Bundala, Kahama – Shinyanga.Zaidi ya wagonjwa 15 wa mifupa wamenusurika kufa kufuatia nyumba ya mganga wa tiba asili anayeunga mifupa kwa njia ya kienyeji kuteketea kwa moto wakati wakiendelea kupatiwa matibabu katika mtaa wa Mbulu Misheni manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Wakizungumza na Jambo Fm baadhi ya wagonjwa wamesema kuwa walisikia kelele za watu wakivunja milango na ndipo wakapata msaada wa kubebwa na kutolewa nje wakati moto huo ukielekea kwenye vyumba vyao.

“Ilikuwa hali ya taharuki sana kwani tulisikia kelele za wananchi na wengine walikuja kwenye milango ya vyumba vyetu na kuingia ndani kisha wakaanza kututoa nje wakati moto ukizidi kuja kwenye vyumba vyetu” Amesema Hamis Simon na John Makoye wagonjwa wa mifupa ya miguu walionusurika.
Katika hatua nyingine wamesema kuwa walitumia nguvu kujivuta kwenda nje ili kujiokoa licha ya kwamba wengine walijitonesha majeraha yao wakati wa purukushani za kujiokoa huku wakilalamika kuibiwa mali zao na baadhi ya vijana waliokuwa wanaowakoa.

“Tunashukuru Mungu tumetoka salama changamoto ni wakati wa purukushani za kujiokoa tumejitonesha majeraha yetu yaliyoaza kupona na baadhi yetu tumeibiwa vitu vyetu na vijana ambao walikuwa wanaingia vyumbani kutupa msaada” amesema Hassan Ahmed na Tumaini Duru walionusurika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Misheni Solomoni Ruta amesema kuwa alipata taarifa majira ya saa kumi jioni ndipo akatoa taarifa kwa mamlaka husika na kupata ushirikiano mkubwa toka kwa wananchi ambao katika hatua za awali walijitaidi kuuzima moto huo na kutoa nje vitu vilivyowezekana.

“Nilipata taarifa toka kwa wananchi majia ya saa kumi jioni na tukawataarifu zima moto,na waipokuja wafanya jitihada kwa kushirikiana na wananchi hatimaye kufanikiwa kuuzima moto huu,niwashukuru sana wananchi wa mtaa wa Mbulu Misheni kwa kujitoa kusaidia uzimaji wamoto huu katika hatua za awali na kufanikiwa kutoa nje baadhi ya vitu,” amesema Ruta Mwenyekiti wa mtaa wa Mbulu Misheni.

Akielezea Chanzo cha moto huo Mkaguzi msaidizi wa jeshi la Zima moto na uokoaji Wilaya ya Kahama Hafidhi Omary amesema chanzo cha moto huo ni mmmoja wa wajukuu wa familia hiyo mwenye umri wa miaka 5 kuchezea kiberiti cha gesi kwenye chumba cha bibi yake kwa kukiwasha na kukielekeza kwenye godoro na kusababisha moto huo.
“Tulifika hapa na kuanza kuzima moto huu,tumefanikiwa kuokoa vyumba vinane na vyumba vinne vimeungua kabisa,na baada ya uchunguzi tumebaini chanzo cha moto huu ni mtoto ambaye ni mjukuu wa familia hii kuchezea kiberiti cha gesi kwa kukiwasha na kukielekeza kwenye godoro ndipo moto huo ukawaka.“ Amesema Hafidhi.
Katika hatua nyingine Jeshi la zima moto na uokoaji wilayani Kahama limewataka wananchi kutoa taarfa mara tu moshi unapoanza kutoka kwa kupiga namba ya bure ya 114 badala ya kusubiri uwashide ndiopo watoe taarifa.
“Tuwaombe wananchi toeni taarifa mara tu moto unapoanza kwa kutupigia simu namba 114,msianze kuzima moto ukiwashida ndipo mtoe taarifa,wengine wakati wanazima basi wengine wapige simu kwetu ili tufike haraka eneo la tukio,” amesisitiza Omary.

Wagonjwa walionusurika katika ajali hiyo ni Joseph Mashauzi,George Joseph,Yunge Mnduka,Elius Ephrahim,Rose Raiza,Samson Deus,Roda Tobotobo na Juma Jumanne.
Wengine ni Magembe Magire,Hassan Ahmed,Tumaini Duru,Zephania Silas,Salum Peter,Hamis Simoni na John Makoye.

CHANZO - JAMBO FM
Social Plugin