Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Katika jitihada za kuinua ubora wa elimu nchini, walimu zaidi ya 3,000 kutoka shule za awali, msingi na sekondari wameingia kwenye kinyang'anyiro cha kitaifa cha kuonesha ubunifu na umahiri wa ufundishaji, huku washindi wakitarajiwa kuondoka na zawadi za mamilioni ya fedha pamoja na vifaa vya kisasa vya kufundishia.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuwa Shindano la Kitaifa la Stadi za Ufundishaji kwa mwaka 2026 litafanyika Juni 6 katika Ukumbi wa Maktaba Mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, likiwa ni toleo la nne kwa walimu wa shule za awali na msingi na la pili kwa walimu wa shule za sekondari Tanzania Bara.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema shindano hilo linaloratibiwa kwa ushirikiano kati ya Wizara na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha mbinu bora za ufundishaji na ujifunzaji nchini.
Amesema kupitia shindano hilo walimu wanapata nafasi ya kuonesha ubunifu wao darasani, kubadilishana uzoefu na kuibua mbinu zinazoweza kuongeza uelewa wa wanafunzi na kuboresha matokeo ya kujifunza.
“Shindano hili ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) unaolenga kuongeza uwezo wa walimu na kuimarisha ubora wa elimu nchini,” amesema.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo, jumla ya walimu 3,153 walijisajili kushiriki kupitia Mfumo wa Kielektroniki wa National Teaching Skills Competition System (TSCS), ambapo walimu 1,263 walikidhi vigezo kwa kuwasilisha video za ufundishaji pamoja na maandalio ya masomo kwa ajili ya tathmini.
Profesa Nombo amesema washiriki wa mwaka huu wanashindana katika maeneo saba ambayo ni Kusoma kwa Darasa la Awali, Kiingereza Darasa la Kwanza, Ufaraguzi wa Zana Darasa la Pili pamoja na masomo ya Physics, Mathematics, Business Studies na Computer Science kwa upande wa shule za sekondari.
Amesema maeneo hayo yamechaguliwa kwa kuzingatia mchango wake katika kuimarisha stadi za kusoma, kuandika kuhesabu, kukuza ujasiriamali, kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiingereza na kuongeza umahiri katika sayansi, hisabati na teknolojia.
Mbali na kutambua walimu bora, shindano hilo pia linatarajiwa kusaidia kueneza mbinu za kisasa za ufundishaji kupitia mifumo ya kidijitali ili walimu wengine nchini waweze kujifunza na kuzitumia katika madarasa yao.
Kwa upande wa zawadi, mshindi wa kwanza katika kila eneo atajinyakulia Sh milioni 2.5, kompyuta mpakato pamoja na vyeti vya ushindi na pongezi, huku shule anayofundisha ikikabidhiwa projekta kwa ajili ya kuimarisha mazingira ya kujifunzia.
Aidha, video za washindi wote wa nafasi ya kwanza zitatayarishwa upya katika studio za TET na kupakiwa kwenye Mfumo wa Elimu wa Kidijitali (LMS) pamoja na kurushwa kupitia TET Soma Kwanza TV, hatua inayolenga kusambaza mbinu bora za ufundishaji kwa walimu kote nchini.
Shindano la mwaka huu limebeba kaulimbiu isemayo, “Ufundishaji Bora, Taifa Imara,” ikisisitiza nafasi ya mwalimu katika kujenga kizazi chenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa.


Social Plugin