Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI WA ULINZI WA KENYA ASISITIZA USHIRIKIANO WA KIJESHI KULINDA AMANI EAC

 

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kenya, Soipan Tuya, amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuendelea kuimarisha ushirikiano, mshikamano na maandalizi ya pamoja katika kukabiliana na vitisho vya kiusalama, majanga mbalimbali, pamoja na changamoto zinazoweza kuhatarisha amani na utulivu wa kikanda. 

Kauli hiyo ameitoa jijini Nairobi, Kenya, wakati wa kufunga zoezi la 14 la pamoja lijulikanalo kama Ushirikiano Imara 2026, ambalo limehitimishwa kwa mafanikio makubwa likihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na majeshi ya nchi wanachama.

Hafla hiyo ya kufunga zoezi hilo ilihudhuriwa pia na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Salum Haji Othman, aliyemwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda. 

Zoezi hili la kimkakati lilijikita katika maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo Operesheni za Kusaidia Amani (PSO), mapambano dhidi ya ugaidi (CT), kukabiliana na uharamia baharini (CP), pamoja na usimamizi wa maafa (DM) kwa lengo la kujenga uwezo wa pamoja wa kiulinzi.

Mkusanyiko huo mkubwa wa kijeshi umewakutanisha washiriki zaidi ya 400 kutoka nchi za Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Ushiriki huu wa mataifa yote nane unalenga kuimarisha utayari, mshikamano na uwezo wa vikosi vya ulinzi na usalama vya EAC ili viweze kukabiliana kwa pamoja na matishio yote ya kiusalama yanayolinyemelea eneo la Afrika Mashariki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com