Shirika lisilo la kiserikali la World Vision limeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha afya na ustawi wa jamii kupitia uhamasishaji wa ujenzi na matumizi ya vyoo bora pamoja na unawaji mikono kwa maji safi, salama na tiririka na utunzaji taka ngumu.
Hayo yamejiri katika kikao cha uhamasishaji wa ujenzi na matumizi ya vyoo bora na unawaji mikono kilichofanyika Juni 1, 2026 katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Hospitali ya Dkt. Jakaya Kikwete wilayani Kishapu, mkoani Shinyanga.
Akifungua kikao hicho, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Fatma Mohamed, amelipongeza Shirika la World Vision kwa kuendelea kuunga mkono maono ya Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta za elimu, afya, mazingira na maji.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora na imara, jambo ambalo linaanza kwa kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora na wananchi wanazingatia unawaji mikono kwa maji safi na salama.
"Afya bora inaanzia kwenye matumizi ya choo bora na unawaji mikono kwa maji safi, salama na tiririka. Hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kutambua wajibu wake katika kulinda afya yake na ya jamii kwa ujumla," amesema Fatma.
Aidha, amewataka watendaji wa vijiji na kata zote nne zinazotekeleza mradi huo chini ya WorldVision ambazo ni Mwakipoya, Shagihilu, Lagana na Ngofila kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kusimamia utekelezaji wa sheria ndogo za halmashauri zinazohusu matumizi ya vyoo bora kwa kila kaya.
Katibu Tawala wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Fatma Mohamed akizungumza kwenye kikao cha uhamasishaji wa ujenzi na matumizi ya vyoo Bora, unawaji mikono na utunzaji wa taka ngumu kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa hospitali ya Dkt. Jakaya Kikwete Wilayani humo akiwa ndiye mgeni rasmi kilichoratibiwa na Shirika la WorldVision Juni Mosi, 2026
"Uwepo wetu hapa sote ni kielelezo kwamba tuna wajibu wa kuhakikisha ajenda ya kila nyumba kuwa na choo inatekelezwa kwa asilimia 100 kama vile WordVision walivyolichukulia suala hili kwa umuhimu na uzito mkubwa vivyo hivyo imetupasa na sisi" ameongeza.
Pia amezikumbusha taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha yanashirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kabla ya kuanzisha au kutekeleza miradi mbalimbali ili kuhakikisha miradi hiyo inawafikia wananchi wenye mahitaji makubwa zaidi.
World Vision Yaahidi Kuendelea Kusimamia Mabadiliko ya Jamii
Kwa upande wake Afisa mradi wilayani Kishapu, akizungumza kwa niaba ya Meneja wa WorldVision Kishapu, Simoni Sylvernus, amesema shirika hilo limewekeza rasilimali kubwa katika mradi huo kwa lengo la kuhamasisha mabadiliko ya tabia na kuondoa dhana potofu kuhusu matumizi ya vyoo bora na vya kisasa.
Amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika Kata nne za awali za mradi huo, bado kuna haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi wa kata, vijiji, viongozi wa dini na vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa.
"Tunapaswa kuendelea kutoa elimu, kusimamia sheria na kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kufikia mwisho wa mradi huu tuweze kuona mabadiliko makubwa katika jamii ya Kishapu," amesema.
Fursa ya Biashara Kupitia Teknolojia ya Vyoo Bora
Akiwasilisha mada kuhusu uhamasishaji wa ujenzi wa vyoo bora kupitia biashara ya choo, Kaimu Afisa Afya wa Wilaya ya Kishapu, Elisha Kapange, amesema mradi huo umeanza kuleta mabadiliko chanya tangu ulipoanzishwa mwaka 2024.
Kapange amesema kumekuwa na ongezeko la wananchi wanaobadilisha vyoo vya asili na kutumia vyoo vya kisasa, huku akitoa wito kwa wanawake, vijana na makundi maalumu kutumia mikopo wanayoipata kuwekeza katika biashara ya vifaa vya kisasa vya choo aina ya SATO.
"Mahitaji ya vifaa hivi yanaongezeka kila siku. Tunawahimiza wanawake, vijana na makundi maalumu kuchangamkia fursa hii ya biashara kwani soko lake linaendelea kukua. Sisi kama wataalamu tupo tayari kuwaelekeza maeneo yenye mahitaji makubwa," amesema Kapange.
Ameongeza kuwa elimu kwa wananchi itaendelea kutolewa ili kupunguza na kuzuia magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na mazingira yasiyo safi, ikiwemo kipindupindu.
Hali ya Matumizi ya Vyoo Bora Katika Kata Zinazotekeleza Mradi
Takwimu zilizowasilishwa katika kikao hicho zinaonyesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kuhamasisha matumizi ya vyoo bora katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo.
Kata ya Mwakipoya: Kaya 1,670 vyoo visivyo bora 292, Kata ya Shagihilu: Kaya 1,076 vyoo visivyo bora 814, Kata ya Lagana: Kaya 1,672 vyoo visivyo bora 1,112, Kata ya Ngofila: Kaya 1,634 vyoo visivyo bora 513.
Mradi huo unatarajiwa kuongeza kasi ya mabadiliko ya tabia kwa wananchi na kuchangia kupunguza magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira kupitia matumizi sahihi ya vyoo bora na unawaji mikono.


Social Plugin