Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imeanza maandalizi ya kupata picha kamili ya sekta ya usafiri wa majini nchini kupitia Sensa ya Vyombo vya Majini na Wajenzi wa Meli Tanzania Bara, hatua inayotarajiwa kuimarisha usalama wa usafiri wa majini, kuvutia uwekezaji na kuongeza mchango wa uchumi wa bluu katika maendeleo ya taifa.
Kupitia sensa hiyo, Tanzania itakusanya kwa mara ya kwanza taarifa za kina kuhusu aina, idadi na hali ya vyombo vya majini vinavyofanya kazi katika bahari, maziwa na mito pamoja na shughuli za ujenzi wa meli nchini.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, amesema takwimu zitakazokusanywa zitakuwa msingi muhimu wa kupanga maendeleo ya sekta ya usafiri wa majini na matumizi bora ya rasilimali za maji ambazo Tanzania imebarikiwa kuwa nazo.
Amesema nchi ina fursa kubwa za kiuchumi kupitia bahari, maziwa makubwa na mito, lakini mafanikio ya kuzitumia kikamilifu yanategemea uwepo wa takwimu sahihi na za kuaminika.
"Sensa hii itatupa taswira halisi ya vyombo vya majini vilivyopo nchini na kutusaidia kutambua maeneo yenye fursa za uwekezaji, kuboresha usafirishaji fungamanishi na kuongeza mchango wa uchumi wa bluu," amesema.
Kwa mujibu wa Dkt. Msengwa, matokeo ya sensa hiyo yataisaidia Serikali kutekeleza kwa ufanisi malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo imeweka mkazo katika ujenzi wa mifumo ya kisasa ya usafirishaji na uchumi shindani.
Amesema maandalizi yote ya zoezi hilo yamekamilika na wataalamu wameandaliwa kuhakikisha ukusanyaji wa taarifa unafanyika kwa viwango vya kitaalamu ili kupata matokeo yenye ubora unaohitajika.
Katika hatua nyingine, wamiliki wa vyombo vya majini wametakiwa kushiriki kikamilifu kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kuijengea nchi kanzidata imara ya sekta hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mohammed Salum, amesema sensa hiyo itakuwa nyenzo muhimu ya kuimarisha usimamizi wa sekta ya usafiri wa majini na kusaidia maamuzi ya muda mrefu ya maendeleo.
Amesema uzoefu wa sensa ya mwaka 2021 ulionesha umuhimu wa takwimu katika kuimarisha usimamizi wa vyombo vya majini nchini.
Kwa mujibu wake, matokeo ya sensa hiyo yaliwezesha TASAC kuongeza wigo wa vyombo vinavyosimamiwa kutoka takribani 6,000 hadi zaidi ya 21,600, jambo lililosaidia kuimarisha ukaguzi, usalama na utekelezaji wa sheria za usafiri wa majini.
"Sasa tunakwenda hatua nyingine kwa kuhusisha vyombo vya aina zote pamoja na wajenzi wa meli ili kupata taswira kamili zaidi ya sekta nzima," amesema.
Ameeleza kuwa takwimu zitakazopatikana zitasaidia kubaini kiwango cha uzingatiaji wa sheria za usalama, mahitaji ya miundombinu, maeneo yanayohitaji uwekezaji pamoja na changamoto zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo.
Wadau wa uchumi wanaeleza kuwa sekta ya usafiri wa majini ni moja ya maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuchochea biashara, utalii, uvuvi na usafirishaji wa mizigo, hivyo uwepo wa takwimu sahihi unaweza kuwa kichocheo kikubwa cha uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa bluu.
Matokeo ya sensa hiyo yanatarajiwa kuipa Serikali na wadau wengine msingi wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu maendeleo ya sekta ya majini, huku yakifungua fursa mpya za biashara na ajira kwa Watanzania katika miaka ijayo.



Social Plugin