Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JAB YAAMINIKA NA WADAU KUIMARISHA TAALUMA YA HABARI.



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wadau wa sekta ya habari nchini wamesema mfumo wa ithibati ya Waandishi wa Habari umechangia kurejesha heshima, uwajibikaji na weledi katika taaluma ya habari, huku ukisaidia kuweka utaratibu unaotambua umuhimu wa elimu, maadili na viwango vya kitaaluma katika utekelezaji wa majukumu ya kihabari.

Wakizungumza katika mahojiano tofauti, jijini Dar es Salaam wadau hao wameeleza kuwa hatua zinazochukuliwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) katika kusimamia ithibati wa Waandishi wa Habari zimeongeza uelewa kuhusu umuhimu wa taaluma hiyo na kuhamasisha uzingatiaji wa maadili na viwango vya kitaaluma.

Mwandishi wa Habari wa AYO TV, Bakari Chijumba, amesema mfumo wa ithibati umeongeza heshima ya taaluma ya habari na kusaidia kupunguza changamoto zilizokuwa zikijitokeza kutokana na baadhi ya watu kufanya kazi za habari bila kuwa na taaluma husika.

“Kwa muda mrefu kulikuwa na watu waliokuwa wakifanya kazi za uandishi wa habari bila kuwa na taaluma husika. Wakati mwingine hali hiyo ilisababisha upotoshaji wa taarifa na ukiukwaji wa maadili ya taaluma. Uwepo wa ithibati umeweka utaratibu unaosaidia kuhakikisha wanaofanya kazi hii wanazingatia viwango vya kitaaluma,” amesema Chijumba.

Kwa upande wake, Mtangazaji wa TBC1, Alice Shayo, amesema uhuru wa vyombo vya habari unapaswa kwenda sambamba na uwajibikaji na uzingatiaji wa maadili ya taaluma.

“Uhuru wa vyombo vya habari una mipaka yake. Mwandishi wa habari anapaswa kufahamu namna ya kukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa kwa kuzingatia maadili na miongozo ya taaluma,” amesema Shayo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Torch Media, James Salvatory, amesema mfumo wa ithibati umechangia kurejesha heshima ya taaluma ya habari kwa kuweka bayana kuwa uandishi wa habari ni taaluma inayohitaji elimu, ujuzi na weledi kama zilivyo taaluma nyingine.

“Ithibati imeongeza hamasa kwa wataalamu wa habari na kuonesha wazi umuhimu wa taaluma hii katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,” amesema Salvatory.

Kwa upande wake, Afisa Habari Mkuu, Neema Mbuja, amesema taaluma ya habari inahitaji elimu, ujuzi na kuongozwa na kanuni na maadili maalumu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya habari.

“Mara nyingi baadhi ya watu walikuwa wakidhani kuwa kujua kusoma na kuandika pekee kunatosha kuwa mwandishi wa habari, jambo ambalo si sahihi. Taaluma ya habari ina misingi, maadili na miongozo inayopaswa kufuatwa ili kuhakikisha huduma bora ya habari inatolewa kwa wananchi,” amesema Mbuja.

Wadau hao wameeleza kuwa kuendelea kuimarishwa kwa mfumo wa ithibati kutasaidia kukuza uaminifu wa umma kwa vyombo vya habari, kuimarisha uwajibikaji wa waandishi na kuongeza hadhi ya taaluma ya habari nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com