Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AMANI NA UMOJA NI MAENDELEO - DIWANI MBAGALA KUU


Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, Ramadhan Serous, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, kulinda usalama na kuimarisha umoja uliopo nchini ili taifa liendelee kupiga hatua za maendeleo.

Akizungumza na blogi hii Serous amesema kuwa amani ndiyo nguzo muhimu inayowezesha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji na maendeleo, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuilinda na kuitunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

"Ili taifa liweze kupiga hatua na wananchi waendelee na uzalishaji, tunahitaji amani. Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunadumisha usalama na umoja uliopo nchini," amesema Serous.

Aidha, amewahimiza wananchi kuungana na kuachana na mambo yaliyopita yanayoweza kuleta migawanyiko, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na serikali katika kuharakisha maendeleo ya nchi.

"Niwaombe wananchi tuungane pamoja na kuachana na yaliyopita. Huu si muda wa kukumbushana vidonda, bali ni wakati wa kushikamana na kushirikiana katika kujenga taifa letu," amesema.

Amesema Tanzania imejengwa katika misingi ya amani na umoja, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuendelea kuenzi tunu hizo ili kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

"Taifa letu limejengwa katika msingi wa umoja na amani. Tushikamane kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu," amesisitiza Serous.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com