Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAKABIDHI ENEO LA UJENZI WA JENGO LA MAMA NA MTOTO NA MAABARA YA KISASA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SHINYANGA

Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya Volumetric Arch Consultant Ltd, Berno Batinamani (kulia), akikabidhi Hati ya Makabidhiano ya Eneo la Ujenzi (Site Possession Certificate) kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya AMAR Builders Ltd, Vipul Maran, wakati wa hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto la ghorofa tano pamoja na Jengo la Maabara ya Kisasa la ghorofa mbili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, iliyofanyika Juni 5, 2026.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, akionesha ramani ya Jengo la Mama na Mtoto likalojengwa hospitalini hapo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, akionesha ramani ya Jengo la Maabara ya Kisasa litalojengwa hospitalini hapo.

Na Kadama Malunde, Shinyanga

Serikali kupitia Kampuni ya Ushauri Elekezi ya Volumetric Arch Consultant Ltd imekabidhi rasmi eneo la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto la ghorofa tano pamoja na Jengo la Maabara ya Kisasa la ghorofa mbili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, hatua inayofungua rasmi utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuboresha huduma za afya mkoani humo.

Makabidhiano hayo yaliyoambatana na utoaji wa Hati ya Makabidhiano ya Eneo la Ujenzi (Site Possession Certificate) yamefanyika leo Ijumaa Juni 5, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, yakihusisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya, wataalamu wa ujenzi pamoja na mkandarasi anayetekeleza mradi huo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya Volumetric Arch Consultant Ltd, Berno Batinamani, amesema mradi huo unatarajiwa kuanza rasmi Juni 19, 2026 na kukamilika mwaka 2028, ukiwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 22.

Amesema majengo hayo yatakapokamilika yataongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za kisasa za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo ya jirani.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni Meneja wa Mkataba wa mradi huo, Festo Mapunda, amemtaka mkandarasi kuhakikisha kazi inatekelezwa kwa ubora unaotakiwa, kwa wakati uliopangwa na kwa gharama zilizokubaliwa kwenye mkataba.

Mapunda pia amesisitiza umuhimu wa kutumia nguvu kazi kutoka kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ili kuwawezesha kunufaika na fursa za ajira zitakazotokana na utekelezaji wa mradi huo.

“Tunatarajia kuona mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika. Aidha, wananchi wa Shinyanga wanapaswa kupewa kipaumbele katika ajira za muda zitakazopatikana wakati wa ujenzi,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya AMAR Builders Ltd, mkandarasi anayejenga majengo hayo, Vipul Maran, amesema kampuni yake imejipanga kikamilifu kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vyote vya kitaalamu vinavyohitajika.

Amesema maandalizi ya awali ya utekelezaji wa mradi yamekamilika na kwamba wataendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na mshauri mwelekezi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa mafanikio.

Kwa upande wake, Mshauri Mwelekezi Berno Batinamani amesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotarajiwa, sambamba na kuhakikisha thamani ya fedha za umma inaonekana kupitia miundombinu itakayojengwa.

Akizungumza kwa niaba ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. John Luzila, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya kupitia miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma za matibabu nchini.

Dkt. Luzila amesema Jengo la Mama na Mtoto litakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 162 kwa wakati mmoja, hatua itakayosaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika mkoa huo.

Aidha, amesema jengo jipya la maabara ya kisasa lenye ghorofa mbili litaboresha huduma za uchunguzi na vipimo mbalimbali vya kitabibu, hivyo kuwawezesha wananchi kupata huduma nyingi za vipimo katika eneo moja bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Ameongeza kuwa, mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya afya nchini kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma bora za kisasa na zinazokidhi mahitaji ya wananchi, sambamba na kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji huduma katika hospitali za rufaa za mikoa.
Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya Volumetric Arch Consultant Ltd, Berno Batinamani (kulia, akikabidhi Hati ya Makabidhiano ya Eneo la Ujenzi (Site Possession Certificate) kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya AMAR Builders Ltd, Vipul Maran, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mkurugenzi wa Kampuni ya AMAR Builders Ltd, mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto pamoja na Maabara ya Kisasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Vipul Maran, akizungumza.
Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya Volumetric Arch Consultant Ltd, Berno Batinamani, akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto pamoja na Maabara ya Kisasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya na Meneja wa Mkataba wa mradi huo, Festo Mapunda, akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto pamoja na Maabara ya Kisasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya na Meneja wa Mkataba wa mradi huo, Festo Mapunda, akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto pamoja na Maabara ya Kisasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila(kulia) akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto na Maabara ya Kisasa hospitalini hapo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com