Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro, amesema utulivu na amani iliyopo nchini Tanzania imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali kuja kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.
Mtatiro ameyasema hayo baada ya kutembelea mradi wa maji uliotekelezwa katika Kijiji cha Zumve Kata ya Nyamalogo Wilaya ya Shinyanga, ambapo amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kulinda amani na kuhakikisha maendeleo yanaendelea kupatikana.
Amesema wananchi wanapaswa kuwa raia wema wanaotekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na serikali pamoja na kuhoji kwa njia sahihi ili kuhakikisha serikali inatimiza wajibu wake kwa wananchi.
“Tukiendelea kuwa wananchi wema ambao tunafanya kazi na serikali yetu, tunaihoji serikali yetu na kuhakikisha inatimiza wajibu wake kwa wananchi na kulinda amani yetu tutaendelea kuvutia wawekezaji wengi zaidi,” amesema Mtatiro
Ameeleza kuwa wawekezaji hawawezi kupeleka mitaji yao katika nchi zenye migogoro na ukosefu wa utulivu, hivyo amani ni rasilimali muhimu inayopaswa kulindwa na kila Mtanzania wakati wote.
“Hawawezi kupeleka uwekezaji kwenye nchi ambazo zina migogoro hivyo amani ni jambo la msingi sana, tuilinde amani yetu usiku na mchana,” amesisitiza Mtatiro
Mtatiro amesema kuwa ulinzi wa amani utasaidia kuvutia miradi mingi ya maendeleo kama mradi wa maji wa Zumve uliotekelezwa na shirika la Water for Good kwa kushirikiana na RUWASA, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi
Social Plugin