Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameeleza utekelezaji wa mradi wa Kituo cha Kisasa cha Uhakiki cha Misugusugu–Kibaha kinachosimamiwa na Wakala wa Vipimo (WMA).
Waziri Kapinga amesema Wakala wa Vipimo ilianzisha ujenzi wa kituo hicho katika eneo la Misugusugu lenye ukubwa wa hekta 2.4, ambapo ujenzi wake umekamilika na kugharimu Shilingi bilioni 7.3.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara Bungeni leo Mei 22, 2026 jijini Dodoma,amesema mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kusogeza huduma za vipimo karibu na wananchi na wadau wa biashara pamoja na kuimarisha miundombinu ya uhakiki nchini.
Kituo hicho kitahusika na uhakiki wa matenki ya magari yanayosafirisha vimiminika, mita mpya za umeme na dira za maji kabla ya kufungwa kwa watumiaji, ili kuhakikisha vifaa hivyo vinakidhi viwango na kutoa matokeo sahihi.
Hata hivyo, Wakala wa Vipimo unakabiliwa na changamoto ya mwitikio hafifu wa baadhi ya wazabuni wa mita za umeme kutotekeleza takwa la kisheria la kuhakiki mita kabla ya kuzipeleka sokoni, pamoja na madai ya muda mrefu ya malipo ya huduma za uhakiki wa dira za maji.
HALI YA UZINGATIAJI WA USHAURI WA KAMATI YA BUNGE
Wakati wa uchambuzi wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara ilitoa maoni na ushauri mbalimbali kwa Wizara.
Serikali imeeleza kuwa imezingatia kwa sehemu kubwa ushauri huo, ingawa baadhi ya miradi kama Magadi Soda–Engaruka na Liganga na Mchuchuma bado ipo katika hatua za majadiliano ya mikataba ya ubia.
Aidha, Serikali inaendelea kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika viwandani kupitia ujenzi wa njia maalum za umeme (dedicated lines) katika maeneo ya viwanda nchini.

Social Plugin