Na Jackline Minja, Dodoma
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kulinda watoto walio katika mazingira hatarishi ikiwemo watoto yatima, wenye ulemavu pamoja na watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
Akijibu swali bungeni, tarehe 22 Mei, 2026 Mahundi amesema Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili (MTAKUWWA II – 2024/25–2028/29), imeendelea kuimarisha huduma za malezi, ulinzi na usalama wa watoto nchini.
“Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara imesajili jumla ya Makao ya Watoto 29 na kuhuisha leseni za makao 39 yenye watoto 855, hali inayofanya jumla ya makao ya watoto kufikia 433 yanayohudumia watoto 16,130 nchini, aidha, jumla ya vituo 809 vya kulelea watoto wadogo mchana vimesajiliwa na vinaendelea kutoa huduma kwa watoto 27,270 nchini. amesema Mhe. Mahundi
Aidha akijibu swali lingine Mhe. Mahundi amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha wanawake wajasiriamali wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika nguzo ya kwanza ya uchumi imara, jumuishi na shindani pamoja na nguzo ya pili ya uwezo wa watu na maendeleo ya jamii.
Akizungumzia watoto wanaolala katika stendi za mabasi na maeneo mengine ya mijini, Naibu Waziri huyo amesema Serikali imeanzisha madawati 14 ya huduma za ustawi wa jamii katika vituo vya usafirishaji ili kushughulikia changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.
Amesema Maafisa Ustawi wa Jamii wamekuwa wakiwahudumia watoto hao kwa kuwahoji na kupata taarifa pamoja na mawasiliano ya wazazi au ndugu zao ili kuhakikisha wanarudishwa kwenye familia zao na kupata malezi stahiki.

Social Plugin