Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YASISITIZA UBORA WA BIDHAA, TBS YAKAMILISHA VIWANGO 230 NA KUTOA LESENI 856 NCHINI



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa ubora wa bidhaa nchini kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ambalo limefanikiwa kukamilisha viwango 230 na kusambaza leseni 856 za nembo ya ubora kwa wazalishaji mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni, Waziri Judith Kapinga amesema juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinazingatia viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa, hususan katika sekta za kilimo, chakula na uhandisi.

Amesema hadi kufikia Aprili 2026, TBS ilikuwa imekamilisha viwango 230, huku viwango vingine 499 vikiwa katika hatua za mwisho za maandalizi, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa mfumo wa ubora wa bidhaa nchini ifikapo mwaka 2026.

Kwa upande wa utoaji wa leseni za nembo ya ubora, Waziri Kapinga amesema jumla ya leseni 856 zimetolewa, sawa na asilimia 85.6 ya lengo la kutoa leseni 1,000 kwa mwaka. Hii inaonesha mwitikio chanya wa wazalishaji katika kuzingatia taratibu za ubora.

Aidha, kati ya leseni hizo, 349 zimenufaisha wajasiriamali wadogo wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa kama siagi ya karanga, asali, maji ya kunywa, mchele pamoja na bidhaa nyingine mbalimbali, hatua inayolenga kuwawezesha kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.

Vilevile, TBS imeendelea kutoa mafunzo kwa wazalishaji na wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuzingatia mifumo ya ubora ili kuhakikisha bidhaa zinazofika kwa watumiaji zinakuwa salama na zenye viwango stahiki.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema hadi Aprili 2026, jumla ya bidhaa 2,070 za chakula na vipodozi zilikuwa zimesajiliwa, sawa na asilimia 86.3 ya lengo la kusajili na kutoa vibali 2,400 kwa mwaka. Kati ya hizo, bidhaa 1,406 ni za chakula na 664 ni za vipodozi, hatua inayolenga kulinda afya za wananchi na kuongeza uaminifu wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com