
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Zuhura Yunus amelishauri Baraza la Vyama vya Siasa kuwa daraja la kuimarisha mahusiano baina ya serikali na makundi ya kijamii ili kulinda amani, umoja na mshikamano wa taifa.
Naibu katibu mkuu huyo alisema hayo mkoani Morogoro wakati akifungua kikao cha kamati ya Uongozi ya baraza hilo.
Alibainisha kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameanzisha wizara hiyo mahususi ili kujenga mahusiano mazuri kwa makundi mbalimbali nchini, huku akiongeza kuwa baada ya kikao hicho viongozi hao watakuwa na uelewa wa pamoja na kuwa mabalozi wazuri wa kuimarisha mahusiano hayo.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisisitiza kuwa viongozi wa vyama vya siasa wana wajibu mkubwa wa kulinda tunu ya amani kwa kuwa wana wafuasi wengi wanaowasikiliza.
Alieleza kuwa ni vyema kuhakikisha wanatunza amani, umoja na mshikamano ulioasisiwa na waasisi wa taifa, Hayati Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatib aliongeza kuwa idara hiyo ya mahusiano itasaidia kutatua changamoto mbalimbali kwa njia ya mazungumzo na kueleza mkakati wao wa kutoa elimu kwa vijana kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili iwasaidie kiuchumi badala ya kuchafua taswira ya nchi.
Mjumbe wa kamati ya uongozi ya baraza hilo na Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu alipongeza kuanzishwa kwa idara hiyo akitaja kuwa ni hatua sahihi wakati huu ambapo taifa linahubiri amani na maridhiano.
Mwalimu alihitimisha kwa kueleza kuwa mahusiano mema ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya nchi, akitolea mfano utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ambayo inahitaji watanzania kuzungumza lugha moja ili kurahisisha mafanikio yake.
Social Plugin