Na mwandishi wetu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Patrobas Katambi amewausia vijana wa Tanzania kuilinda amani iliyopo na kuwausia kuwa na malengo kwani Taifa linawategemea kuwa viongozi wa kesho katika nafasi mbalimbali za kiuongozi.
Waziri Katambi ameyasema hayo wakati akifungua Mada ya Amani na Usalama katika Jukwaa la Maendeleo ya Vijana Tanzania,jijini Dodoma ambapo jumla ya Vijana 600 kutoka mikoa mbalimbali nchini wamekutana kuadhimisha Miaka Mitano ya Jukwaa la Maendeleo ya Vijana.
“Ili uwe kijana mwenye staha na kijana mwenye mafanikio ni vizuri sana tukajua sheria za nchi yetu na tukazitii na tukawasaidia wengine kuzijua sheria za nchi yetu,vijana wengi wamekua wanakumbwa na matatizo kwa kufanya mambo au vitendo vinavyompelekea kupata madhira”amesema Waziri Katambi
Waziri Katambi amekemea pia tabia ya siasa za uchochezi,siasa zinazohamasisha vurugu,siasa za kuwatenga watu huku akiwaasa vijana kutowapa nafasi watu wenye mlengo wa siasa za kuligawa taifa.
Kuhusu utoaji wa taarifa za uhalifu Waziri Katambi amewaasa vijana kutoficha taarifa,kutowaficha waharifu ambapo aliweka wazi wahalifu kupatikana ndani ya jamii tunazoishi na endapo wakiachiwa wanaweza kuleta madhara ambayo hakuna mtu ataachwa salama.
Vijana hao pia waliaswa kutumia elimu waliyonayo kuwaelewesha wenzao juu ya kuilinda nchi ya Tanzania kwani hakuna nchi nyingine zaidi ya nchi waliyopo na waliyozaliwa na taifa linawategemea kuwa viongozi wa baadae.
“Nawasihi mtumie vizuri mitandao ya kijamii,muitumie kujua taarifa mbalimbali za afya,fursa za kiuchumi na kujua mataifa yanayoendelea Njia gani wanatumia katika kujiletea maendeleo,nawaomba msitumie mitandao kutukana watu,kudhalilisha watu,uzushi,kueneza chuki na kueneza ubaguzi”amesema Waziri Katambi

Social Plugin