Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YA SAMIA YAJENGA KM 243 ZA BARABARA ZA LAMI NDANI YA MIEZI 10



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Jumla ya Kilometa 243.13 za barabara za lami zimejengwa nchini ndani ya miezi 10 kuanzia Julai 2025 hadi Aprili 2026, huku Serikali ya Awamu ya Sita ikiendelea kuongeza kasi ya uboreshaji wa miundombinu ya usafiri kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma leo Mei 20, 2026, Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema katika kipindi hicho Serikali pia imekarabati kilometa 94.36 za barabara kwa kiwango cha changarawe.

Ulega amesema mtandao wa barabara za kitaifa unaosimamiwa na TANROADS umefikia kilometa 37,734.41 ambapo kilometa 12,225.26 tayari zimejengwa kwa kiwango cha lami, hatua inayotajwa kuongeza ufanisi wa usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini.

Amesema tangu mwaka 1961 wakati Tanzania inapata uhuru, nchi ilikuwa na kilometa 1,360 pekee za barabara za lami, huku kuanzia Serikali za Awamu ya Kwanza hadi ya Tano zikijengwa kilometa 9,369.81.

Aidha, amesema ndani ya miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, jumla ya kilometa 1,495.45 za barabara pamoja na madaraja makubwa 18 yamejengwa.

Katika hatua nyingine, Ulega amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa madaraja makubwa tisa, huku ujenzi wa madaraja 11 ukiendelea na maandalizi ya ujenzi wa madaraja 13 yakiendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo umeendelea kufungua maeneo ya uzalishaji, biashara na uwekezaji sambamba na kuongeza ufanisi wa sekta nyingine za usafiri ikiwemo reli, bandari na viwanja vya ndege.

Pia amesema Serikali imeendelea kulinda uwekezaji wa miundombinu hiyo kwa kufanya matengenezo ya mara kwa mara ambapo kilometa 16,782.58 za barabara zimefanyiwa matengenezo ya kawaida, kilometa 1,101.12 matengenezo ya muda maalum pamoja na matengenezo ya sehemu korofi kwa kilometa 147.13 huku madaraja 1,383 yakifanyiwa matengenezo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com