Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RIPOTI YA JAJI CHANDE IMEELEZA MAHITAJI YA WANANCHI- CHAUMMA



Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu amesema Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imetekeleza wajibu wake kikamilifu kulingana na mahitaji ya Watanzania, akisema Kamati kuu ya Chama hicho imeridhika na vyanzo vilivyotolewa kama sababu ya watu kufanya ghasia hizo.

"Jaji Chande amesema kuhusu Katiba mpya, amesema kuhusu Tume huru ya uchaguzi, amezungumzia suala la uchumi wa vijana na hali ya ajira, amezungumza kuhusu suala la utekaji na watu kupotea na Jaji Chande amezungumza pia kuhusu uwajibikaji hafifu wa Viongozi katika kuwatumikia Wananchi. Sisi hatuna mashaka na mambo haya na hakuna anayeweza kukataa kuwa vile vilivyozungumzwa si kero kwa Watanzania." Amesema.

Mwalimu amebainisha hayo leo Alhamisi Mei 07, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam kuhusu maazimio ya Kamati kuu ya CHAUMMA kuhusu ripoti ya Oktoba 29, 2025 kutoka kwenye Tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Othman Chande.

"Kama hizo ndio kero zetu tunazipinga ili iweje? Sisi tumeukataa huo mtego na badala ya kuipinga ripoti ile tumeelekeza nguvu zetu kushinikiza serikali kufanyia kazi yale yaliyozungumzwa na Jaji Chande kuliko kuanza kupinga na hapa ndipo wakati mwingine tunapaswa kujiuliza huwa tunakosea wapi sisi kama Wapinzani?anahoji,

Ameongeza, "Katiba tumeidai kwa zaidi ya miaka 30 na Tume zimeundwa nyingi na zimezungumza kuhusu mambo haya, sasa sisi huwa tunakosea wapi? Nadhani moja ya sababu ni kutanguliza ile dhana wapinzani kazi yao ni kupinga tu kila kitu na badala yake tunaanza tena kutumia ripoti hizi hizi kama rejea. Hata wanaoipinga ripoti hii ya Jaji Chande ipo siku wataitumia kama rejea ya masuala mbalimbali, "ameeleza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com