Na Dotto Kwilasa, Dodoma, Mei 06, 2026
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha sekta ya elimu nchini kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya shule, lengo likiwa ni kuinua ubora wa elimu na kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika ngazi zote.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Riziki Shemdoe, wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Elimu 2026 uliofanyika katika Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.
Akizungumza katika mkutano huo, Prof. Shemdoe amesema maboresho ya miundombinu ya elimu yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ufaulu katika mitihani na upimaji wa kitaifa kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi sekondari.
Ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha shule zinakuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, jambo ambalo limeleta matokeo chanya kwa wanafunzi na walimu.
Aidha, Waziri Shemdoe amewapongeza walimu, wanafunzi na wadau wa elimu kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha taaluma nchini. Amesema ushirikiano wao umechangia kwa kiasi kikubwa kuinua viwango vya elimu, hususan katika Mkoa wa Dodoma ambao umeendelea kufanya vizuri kitaaluma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Mkoa huo umefikia hatua ya kihistoria kwa kushika nafasi ya pili kitaifa katika matokeo ya kitaaluma mwaka 2025.
Amefafanua kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano imara kati ya Serikali, walimu, wazazi na wadau wa elimu pamoja na utekelezaji wa mikakati madhubuti ya kuboresha sekta ya elimu.
Katika kipengele cha Elimu kama msingi wa maendeleo
Senyamule amesema,Serikali imeendelea kusisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, huku ikihimiza wadau wote kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha vijana wanapata elimu bora itakayowawezesha kushindana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.
Amesema Dodoma inaendelea kuwa mfano wa mafanikio ya kielimu nchini, ikiwa ni ishara ya matokeo chanya ya sera na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya elimu.




Social Plugin