
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kumbukizi ya miaka mitano ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, iliyofanyika Kilimani, Chato mkoani Geita leo tarehe 17 Machi 2026.
Maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa la kutathmini na kuenzi misingi ya uthubutu, ujasiri, na uzalendo uliotukuka ambao Hayati Magufuli aliishi katika kipindi chote cha uongozi wake.
Salamu za Serikali na Wito wa Kazi
Akitoa salamu za Serikali, Makamu wa Rais amesema ili kumuenzi Hayati Magufuli kwa vitendo ni vyema kila Mtanzania kujifunza wito wa kujitoa na kufanya kazi kwa bidii. Amesema Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliyejitambulisha kwa Falsafa yake ya “Hapa Kazi tu”, alitaka kila mtu kujituma na kutoa mchango wake kwa Taifa kwa njia ya kazi, akiamini kuwa hiyo ndiyo njia pekee inayoweza kuondoa umaskini katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, kaya na hata Taifa kwa ujumla.
Makamu wa Rais amebainisha kuwa funzo kutoka kwa Hayati Dkt. Magufuli ni ujasiri na uthubutu wake katika kufanya maamuzi magumu na yenye manufaa kwa Taifa. Ameongeza kwamba alifundisha umuhimu wa kuwajibika na kusimamia misingi ya haki na usawa, huku akiwa hakuyumbishwa katika kupiga vita uzembe na rushwa. Aidha, amesisitiza kuwa Hayati Magufuli alifundisha kuwa hatima ya Tanzania na Afrika iko mikononi mwa Watanzania na Waafrika wenyewe kupitia ulinzi wa rasilimali.
Maisha ya Darasa na Ujenzi wa Makumbusho
Dkt. Nchimbi ameeleza kuwa maisha ya Hayati Magufuli yalikuwa ni darasa zuri kwa viongozi, ambapo kupitia uongozi wake aliweza kulea na kuinua viongozi wapya wengi, hasa vijana. Katika hatua nyingine, amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akifuatilia kwa karibu ujenzi wa makumbusho ya Hayati Magufuli yaliyopo Chato, na kuamua kutoa shilingi milioni 100 zilizobaki ili kukamilisha ujenzi huo kama sehemu ya kuenzi urithi wake.
Salamu za Rais wa Zanzibar na Familia
Kumbukizi hiyo imehudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye amesema namna bora ya kumuenzi Hayati Magufuli ni kuendeleza dhamira yake ya kuhimiza uwajibikaji, kuwajali wanyonge, na kulinda rasilimali za nchi. Amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kusimamia na kuhakikisha maono ya Hayati Magufuli yanatimizwa kwa vitendo.
Kwa niaba ya familia, Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Jesca Magufuli, ameishukuru Serikali kwa namna inavyoendelea kuhifadhi kumbukumbu za Hayati Dkt. Magufuli kwa heshima na staha. Familia imempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano alioutoa kwa familia katika kipindi chote cha miaka mitano pamoja na kuendeleza kazi za ujenzi wa Taifa.
Harambee ya Maendeleo
Katika Kumbukizi hiyo, jumla ya kiasi cha shilingi milioni 474, ikiwemo ahadi na fedha taslimu, zimekusanywa katika harambee iliyoongozwa na Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa lengo la kumalizia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Kilimani Wilayani Chato.



Social Plugin