Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA USULUHISHI KUAMUA MZOZO WA RWANDA NA UINGEREZA



THE HAGUE, Uholanzi

Mzozo mkubwa wa kisheria kati ya serikali ya Rwanda na Uingereza kuhusu makubaliano ya hifadhi ya wakimbizi yaliyoshindwa kutekelezwa, unatarajiwa kuanza kusikilizwa Machi 18,2026, katika Mahakama ya Kudumu ya Usuluhishi (PCA) jijini hapa.

Rwanda ilianzisha mchakato huo wa kusaka usuluhishi Januari mwaka huu, ikilalamikia kukiukwa kwa mkataba (MEDP) baina ya nchi hizo uliotiwa saini mwaka 2024.

Makubaliano hayo yanalenga kuweka utaratibu ambapo Uingereza ingewahamishia Rwanda baadhi ya wakimbizi walio katika mazingira magumu zaidi. Ingawa mkataba huo uliweka mfumo mkuu wa ushirikiano, maelezo ya kina hayakuwahi kukamilishwa hadi serikali mpya ya Uingereza ilipotangaza kusitisha ushirikiano huo mwaka jana.

Katika shauri hilo, Rwanda inaishitaki Uingereza kwa kushindwa kutimiza ahadi zake kulingana na mkataba. Wizara ya Sheria ya Rwanda imeeleza kuwa, kupitia makubaliano hayo ya kidiplomasia ya Juni 2024, nchi hizo mbili zilikubaliana mipango ya kifedha kusaidia ugharamiaji wa wakimbizi na miradi ya kiuchumi.

Chini ya makubaliano hayo, malipo mawili ya kiasi cha pauni milioni 50 kila moja (takriban bilioni 150 za Kitanzania kila moja) yalipaswa kutolewa kati ya Aprili 2025 na Aprili 2026. Hata hivyo, wizara hiyo inasema malipo hayo hayajafanyika.

Rwanda inasema ingawa serikali mpya ya Uingereza ilitangaza kusitisha ushirikiano huo, ilifanya hivyo kabla ya kufuata taratibu rasmi za kusitisha mkataba huo kisheria.

Kesi hii katika mahakama ya The Hague inasubiriwa kwa hamu ili kuona kama Uingereza italazimika kulipa mabilioni hayo ya fedha licha ya kujiondoa kwenye mpango huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com