Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIPO, BRELA NA COSTECH WAZINDUA MRADI WA TEKNOLOJIA KUONGEZA THAMANI YA MAZAO


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Dunia la Haki Miliki (WIPO) kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, wamezindua mradi wa miezi 12 utakaotumia teknolojia zilizopo kwenye kanzidata za kimataifa za hakimiliki kuongeza thamani ya mazao, kupunguza gharama za uzalishaji na kuimarisha sekta za kilimo na ufugaji nchini.

Mradi huo unalenga kutambua, kuchambua na kuhamisha teknolojia ambazo muda wake wa ulinzi wa hakimiliki umeisha kupitia kanzidata za WIPO, ili ziweze kufanyiwa maboresho kulingana na mazingira na mahitaji ya Tanzania kwa manufaa ya wakulima, wafugaji na sekta ya viwanda.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo leo Juni 1, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuchochea maendeleo ya uchumi, hususan katika sekta za kilimo na ufugaji.

Amesema mradi huo utawezesha wataalamu na wabunifu wa ndani kupata teknolojia sahihi zinazoweza kuboreshwa na kutumika katika uzalishaji wa chakula cha mifugo, uchakataji wa mazao pamoja na maendeleo ya viwanda vinavyotegemea malighafi za kilimo.

“Mradi huu utajikita katika kutafuta teknolojia zinazofaa mazingira ya Tanzania kupitia kanzidata za WIPO, ambapo teknolojia hizo zitafanyiwa maboresho kulingana na mahitaji ya ndani na kutumika kuandaa mifano ya mashine na vifaa vitakavyosaidia kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa za kilimo,” amesema Dk. Nungu.

Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia hizo yatasaidia kupunguza utegemezi wa teknolojia ghali kutoka nje ya nchi, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza mchango wa ubunifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka BRELA, Loy Mhando, amesema mradi huo utasaidia kutumia taarifa zilizopo kwenye kanzidata za kimataifa za hakimiliki kutafuta teknolojia zinazoweza kuongeza tija kwa wakulima na wafugaji, hasa katika uzalishaji wa chakula cha mifugo kwa kutumia mabaki ya mazao ya kilimo.

Amesema matumizi ya teknolojia hizo yatapunguza gharama za uzalishaji, kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Nchi Zenye Maendeleo Duni wa WIPO, Prevdovj Vaanching, amesema taasisi hiyo itaendelea kusaidia nchi zinazoendelea kutumia ubunifu na teknolojia kama nyenzo muhimu za kukuza uchumi na kufanikisha maendeleo endelevu.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Profesa Thomas Kivevele, amesema mradi huo utaimarisha uwezo wa vyuo vikuu na taasisi za utafiti kuunganisha matokeo ya tafiti na mahitaji halisi ya soko, jambo litakalosaidia kuongeza matumizi ya ubunifu katika uzalishaji wa bidhaa na huduma.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika, mkulima na mfugaji kutoka Njombe, Anna Gombela, amesema teknolojia hizo zinatarajiwa kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kuinua kipato cha wakulima na wafugaji, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Mradi huo utaanza kutekelezwa katika mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa, ukielekeza nguvu zaidi katika uzalishaji wa chakula cha mifugo kwa kutumia mabaki ya mazao ya kilimo, hatua inayotarajiwa kuongeza thamani ya mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea uwekezaji katika sekta ya kilimo na ufugaji nchini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com