
Na Hadija Bagasha Tanga,
Jamii imetakiwa kuendelea kushirikiana katika makuzi na malezi ya watoto na vijana ili kujenga kizazi chenye maadili mema, uwajibikaji na uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Katibu wa Taasisi ya MIFTAH SALAAM, Idrisa Modo, wakati wa kongamano la amani lililowakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili masuala ya amani, mshikamano wa kijamii na maendeleo endelevu.
Akizungumza katika kongamano hilo, Modo amesema kuwa malezi bora yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, viongozi wa dini, serikali na wadau wengine wa maendeleo ili kuhakikisha vijana wanalelewa katika misingi ya maadili, uzalendo na uwajibikaji.
Ameeleza kuwa vijana ni nguvu kazi muhimu ya taifa, hivyo wanapaswa kupewa mwongozo sahihi utakaowasaidia kuwa raia wema na wenye mchango chanya katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Aidha, amesema Taasisi ya MIFTAH SALAAM imejipanga kuufikia mkoa mzima wa Tanga kupitia programu mbalimbali za elimu, uhamasishaji na mafunzo yanayolenga kuimarisha amani, mshikamano wa kijamii, maadili mema na maendeleo ya vijana.
Modo amesisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo yoyote, hivyo kuna umuhimu wa wadau wote kushirikiana katika kulea na kuelimisha vijana ili kuwa mabalozi wa amani na maendeleo katika jamii zao.
Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, jamii itaweza kujenga kizazi chenye maono, nidhamu na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri ustawi wa Taifa.







Social Plugin