Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, amewataka watendaji wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai kuendelea kujiimarisha kitaaluma na kutumia teknolojia za kisasa katika kukabiliana na uhalifu unaozidi kutumia mbinu za hali ya juu.
Akifungua Kikao Kazi cha Kuwajengea Uwezo Watendaji wa Kamisheni hiyo katika Shule ya Polisi Tanzania Moshi Jumatatu Juni 1, 2026, IGP Wambura amesema maendeleo ya sayansi na teknolojia yamebadilisha mazingira ya utendaji wa uhalifu, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kutumia mbinu za kisasa katika ukusanyaji na uchambuzi wa ushahidi ili kusaidia upatikanaji wa haki.
IGP Wambura amewapongeza pia watendaji wa Kamisheni hiyo kwa kazi wanayoifanya ya kufika katika maeneo ya matukio, kukusanya ushahidi na kusaidia uchunguzi wa kisayansi, akisisitiza kuwa hakuna uhalifu unaoweza kutendeka bila kuacha ushahidi unaoweza kusaidia kuwabaini wahalifu, hivyo amewataka watendaji hao kuzingatia weledi, uadilifu na kuendelea kujifunza ili kuimarisha utendaji kazi na kuongeza imani ya wananchi kwa mfumo wa haki jinai.
Aidha katika hotuba yake amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuwekeza katika mafunzo na teknolojia za kisasa ikiwemo uchunguzi wa vinasaba (DNA), uchambuzi wa kidigitali na mbinu nyingine za kisayansi, akisema uwekezaji huo unalenga kuifanya Kamisheni hiyo kuwa mhimili imara katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimtandao, uhalifu wa kimataifa na makosa mengine yanayohitaji uchunguzi wa kisasa unaozingatia ushahidi wa kisayansi.
IGP Wambura kadhalika amesisitiza kuwa ushahidi wanaokusanya una mchango mkubwa katika kuwapatia haki waathirika wa uhalifu, kuwawajibisha wahalifu na kujenga imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi na mfumo mzima wa haki jinai. Alieleza kuwa matarajio ya Jeshi la Polisi ni kuona maarifa yatakayopatikana katika kikao hicho yatatutumika kuleta mabadiliko chanya katika utendaji wa watendaji wote wa Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi nchini.

Social Plugin