Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM YAIMARISHA MSIMAMO WAKE KATIKATI YA NJADALA WA KISIASA KWA KUELEKEZA NGUVU KWENYE MALEZI


Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Malezi ya watoto na ujenzi wa maadili kwa kizazi kipya ndiyo yamepewa kipaumbele na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi, ambayo imetangaza kuandaa waraka maalumu utakaolenga kuimarisha makuzi ya watoto kwa kuzingatia mila, desturi na maadili ya Kitanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 4, 2026 jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya Wiki ya Wazazi itakayofikia kilele Julai 4, 2026 mkoani Mwanza, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Fadhili Mganya, amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto za kijamii zinazoathiri malezi ya watoto na vijana.

Amesema waraka huo mpya unalenga kurejesha msisitizo wa jamii katika malezi bora, akisisitiza kuwa malezi si jukumu la wazazi pekee bali ni la jamii nzima inayoshiriki kulea kizazi chenye maadili na uzalendo.

“Kabla ya kilele cha Wiki ya Wazazi tutakuwa na kongamano la kitaifa litakalowakutanisha wadau mbalimbali kujadili malezi, maadili na ustawi wa jamii ili kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha makuzi ya watoto nchini,” amesema Mganya.

Katika hatua nyingine, katikati ya mjadala wa kisiasa unaoendelea nchini, Jumuiya hiyo imesisitiza kuwa chama kinaendelea kuwa imara na chenye mshikamano mkubwa, ikieleza kuwa kauli za mtu mmoja mmoja haziwezi kuwakilisha msimamo rasmi wa chama chenye wanachama zaidi ya milioni 13.

Mganya amesema licha ya kuwepo kwa mitazamo tofauti inayojitokeza mara kwa mara ndani ya ulingo wa siasa, hususan kupitia mijadala ya bungeni na vikao mbalimbali, hali hiyo haitafsiriwi kama mgawanyiko wa chama.

“Mtu mmoja hawezi kuwakilisha msimamo wa CCM. Chama chetu kina wanachama zaidi ya milioni 13 na kina taratibu zake za kutoa msimamo rasmi kupitia viongozi wake wa kitaifa,” amesisitiza.

Kauli hiyo imekuja kufuatia mjadala uliotokana na matamshi ya Mohamed Simai Said wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Fedha, ambayo yaliibua tafsiri tofauti katika anga ya kisiasa.

Hata hivyo, Jumuiya ya Wazazi imesisitiza kuwa chama kinaendelea kusimama imara bila kuyumbishwa na mijadala hiyo, ikibainisha kuwa mfumo wake wa uongozi na maamuzi unaendelea kulinda mshikamano wa ndani.

Kwa mujibu wa Mganya, viongozi wenye mamlaka ya kutoa msimamo rasmi wa chama ni Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu Wenyeviti wa CCM Tanzania Bara na Zanzibar, Katibu Mkuu pamoja na Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo.

Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi mwaka huu yataongozwa na maeneo matano muhimu ambayo ni elimu, malezi na maadili, mazingira, afya na utamaduni, huku shughuli mbalimbali zikitarajiwa kufanyika Tanzania Bara na Zanzibar kwa lengo la kuhamasisha jamii kushiriki katika kujenga kizazi chenye maadili na uzalendo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com