Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAWAPA KIPAUMBELE VIJANA KATIKA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU DAR ES SALAAM


-Ulega asema ni mkakati endelevu

-Walengwa ni waajiriwa wapya na waliojiajiri

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema vijana walioanza ajira karibuni na wale waliojiajiri watapewa kipaumbele katika kupewa nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na Serikali jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa nyumba 144 za gharama nafuu zinazojengwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) Wilayani Temeke jijini Dar es Salaam leo, Ulega alisema Serikali imechukua hatua hiyo kutokana na changamoto ambazo vijana wanazipitia kwenye kupata nyumba za gharama nafuu kuishi.

“Kwa mujibu wa Sensa ya Mwaka 2020, Tanzania ina upungufu mkubwa wa nyumba. Kwa kuzingatia hilo, tumeamua kuanza kuchukua hatua za makusudi kushughulikia changamoto hiyo.

“Nyumba hizi 144 ni hapa Dar es salaam. Lakini Rais wenu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameidhinisha pia ujenzi wa nyumba za namna hii mkoani Dodoma na katika miji mingine mikubwa ili kupambana na changamoto hii,” alisema Ulega.

Kati ya nyumba hizo 144 zinazoendelea kujengwa, 72 ni nyumba za chumba kimoja, sebule, jiko na choo na 72 nyingine ni nyumba za vyumba viwili ambapo kimoja ni self-contained, sebule, jiko na choo cha pamoja (common toilet).

Ulega amesema mpango huu utaendelea kupanuliwa katika mikoa mingine ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana wanapata makazi bora na nafuu kwa awamu na kwa usawa katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na mahitaji.

Waziri Ulega, amesema vijana walioajiriwa na waliojiajiri wanalazimika kukaa mbali na maeneo yao ya kazi kutokana na uhaba wa nyumba, jambo linaloathiri muda wao wa kuchapa kazi.

Alisema kwa kujenga nyumba katika maeneo ya mijini ambako kuna watu na fursa nyingi zaidi, Serikali inaweka mazingira mazuri kwa vijana kutumia muda mwingi zaidi kuchapa kazi badala ya kuhangaika kutafuta nyumba na usafiri.

Waziri huyo aliwaeleza wananchi waliohudhuria tukio hilo kuwa suala la ujenzi wa nyumba za gharama nafuu si la Wizara ya Ujenzi pekee bali ni sehemu ya Mipango ya Muda Mrefu ya Serikali kupitia Dira ya Taifa 2050.

“Mkiona Waziri wa Ujenzi yuko hapa leo si kwa sababu hili ni suala lake binafsi au wizara yake. Suala la nyumba liko kwenye Dira ya Taifa 2050 na hii ni sehemu ya utekelezaji wake,” alisema Ulega.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com