Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AMPA TUZO YA MFANYAKAZI HODARI PROFESA NDUNGURU KWA KUPAISHA MAPATO NA MABORESHO YA TPHPA


Mwandishi Wetu,Njombe

Rais wa Jamuhuri  ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa amempatia tuzo ya cheti na zawadi ya mfanyakazi Hodari ,Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru.

Profesa Ndunguru anatoka   Chama cha wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Tekinolojia, Taasisi za Habari, Vyuo vya Ufundi Stadi, Taasisi za Utafiti (RAAWU) na  alijiunga na TPHPA mwaka mwaka 2023 na tangu amejiunga na taasisi hiyo nyeti nchini,  amefanya mabadiliko makubwa na sasa imekuwa Taasisi ya mfano barani Afrika.

Miongoni mwa mafanikio hayo kuongeza uwezo wa kuchambua viuatilifu, kuboresha maabara  kuwa za kisasa  na kuweza kuzijenga na kuziunganisha katika mfumo mmoja unaosomana  Ofisi 47 zilizopo katika mipaka ya Tanzania, zinazosimamia  upimaji na uingizaji wa   viatilifu   hali iliyoingeza  ufanisi na mapato  kutoka bilioni 14 kwa mwaka 2023 hadi kufikia bilioni 69 kwa miezi minane tu, kuanzia Julai 2025 hadi februari mwaka huu.

Akizungumza katika Sherehe hizo, Rais Samia aliwapongeza wafanyakazi Hodari waliopewa tuzo na wafanyakazi wengine wote nchini kwa kuchapa kazi kubwa ambayo inawezesha kukua kwa Uchumi wa nchi na  kuendelea kuwahakikishia wafanyakazi maslahi bora.

“Chapeni kazi, Serikali inatambua mchango wenu na kila hali ya kiuchumi inapokuwa nzuri tutaendelea kuboresha maslahi yenu,lakini pia tunaendelea kulipa malimbikizo ya madai yenu  na kutafuta fursa nyingi za ajira  zenye staha ndani na nje ya nchi”,alisema.

Profesa Ndunguru akizungumza na waandishi wa Habari baada ya kutangazwa kushinda, alisema ushindi wake, umetokana na ushirikiano mkubwa baina ya TPHPA na Serikali na pia mshikamano baina ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo,kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais Samia Suluhu.

“Mimi ni kiongozi tu na wafanyakazi wenzangu, sote tunajivunia mafanikio ya TPHPA ndani ya miaka mitatu na tumekuwa tukipokea watafiti na wanasanyansi kutoka nchi mbali mbali Afrika kuja kujifunza siri ya mafanikio yetu”,alisema.

Alisema Mamlaka hiyo, sasa imewezesha wafanyabiashara wa mazao ya kilimo ,kuepukana na adha ya kwenda kupima ubora wa bidhaa zao kwa ajili ya masoko ya  kimataifa, katika maabara za nje ya nchi, kwani sasa hapa hapa Tanzania wanapima na kupata ithibati.

“Miaka ya nyuma mazao yetu yalikuwa yanapimwa nchi jirani ili kwenda kuuzwa nje lakini sasa tunapima wenyewe kwani maabara zetu zilizopo maeneo mbali mbali nchini, zinatambulika na zimeidhinishwa kimataifa”,alisema.

Akizungumzia mchango wa Taasisi hiyo kwa wakulima, alisema licha ya kuwasaidia kuzalisha mazao bora yasiyo na chembemchembe za viuatilifu, lakini pia imekuwa ikiwatafutia masoko ya kimataifa hasa kwa mazao ya kimkakati kwa Taifa.

“Kuna kampuni 16 za mazao ya parachichi na viazi mviringo, tumewatafutia masoko  China, lakini pia  wakulima wadogo ya viazi tunawawezesha kusafisha viazi hapa hapa nchini kabla ya kusafirisha nchi za nje”,alisema.

Alisema kwa sasa pia ujenzi wa maabara zaidi unaendelea makao makuu ya TPHPA mkoani Arusha,lakini pia inatarajiwa kujengwa maabara nyingine  katika mji wa Makambako lengo ni kuwezesha wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi yakiwa na ubora unaotakiwa.

Profesa Ndunguru pia alisema, katika kuhakikisha mbegu za asili zinaendelea kuwepo nchini, TPHPA inakusudia kujenga jengo la kuhifadhi mbegu 10,000 za asili ambazo zitakuwa zikitumiwa na wakulima na watafiti.

“Tunakwenda vizuri kwani pia kwa sasa tunauwezo wa kuchambua sampuri 2000 kwa wiki na hivyo, kuondoa ucheleweshwaji wa kuidhinishwa sampuri hizo kwa ajili ya matumizi mbali mbali”alisema.

Profesa Ndunguru pia aliahidi kufanyakazi na chama cha wafanyakazi katika vyombo vya Habari nchini (JOWUTA) kwa kuwajengea uwezo wanahabari juu ya kazi za Mamlaka hiyo, lakini pia kusaidia kufichuwa wanapenyeza vichochoroni viatilifu ambavyo  havijaidhinishwa na Mamlaka hiyo ili kulinda afya za mime ana binaadamu.

Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma alimpongeza Profesa Ndunguru na wafanyakazi wote wa TPHPA Kwa kazi nzuri wanayofanya na pia alishukuru TPHPA kuwa mmoja wa wafadhili wa zawadi za waandishi hodari mwaka 2026.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com