Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATARAJIA ONGEZEKO LA WELEDI KWA MAWAKILI WA SERIKALI

Na Bora Mustafa,Arusha.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Athuman amesema Serikali inatarajia kuona ongezeko la weledi, uwajibikaji pamoja na ufanisi kwa mawakili wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

AkizungumzaLeo mei ,20,2026  jijini Arusha wakati akifunga mafunzo ya mawakili wa Serikali, Zainabu amesema Serikali inaendelea kuwategemea wataalamu hao katika kulinda rasilimali za taifa kupitia ushauri wa kisheria wenye tija pamoja na usimamizi madhubuti wa mashauri mbalimbali.

Pia amesema baada ya mafunzo hayo, mawakili hao wanatarajiwa kusimamia kwa ufanisi mashauri ya Serikali, kuimarisha usimamizi wa mikataba na manunuzi ya umma pamoja na kuishauri Serikali kuhusu sheria za kodi na utatuzi wa migogoro ya ndani na kimataifa.

Hata hivyo, Zainabu amesema hatua hiyo ni muhimu katika kipindi ambacho taifa linaelekea kwenye utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yenye lengo la kujenga uchumi wa kati unaowanufaisha wananchi wote.

Kwa upande wake, Wakili Mkuu wa Serikali Dr Ally Possi amesema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imefanikiwa kuokoa fedha za Serikali kiasi cha trilioni 1.35 kupitia usimamizi wa mashauri mbalimbali ya kisheria.

Aidha, Dr Possi amesema mawakili wa Serikali ni askari wa kalamu wanaolinda utawala bora wa sheria pamoja na uchumi wa nchi, huku akiiomba Serikali kuendelea kuiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Ameongeza kuwa mawakili wa Serikali wamejipanga kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha kila hatua ya maendeleo ya uchumi wa taifa inalindwa kisheria na kusimamiwa kwa weledi mkubwa.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com