Na Dotto Kwilasa, Dodoma
SERIKALI imeanza rasmi mchakato wa maboresho ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 kwa lengo la kuifanya iendane na mabadiliko ya sasa ya kisera, kiteknolojia na mahitaji ya mfumo wa elimu nchini.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maboresho makubwa yanayoendelea kufanywa katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na sera mpya ya elimu, maboresho ya mitaala, ongezeko la walimu pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.
Akizungumza Mei 21, 2026 jijini Dodoma wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya awali ya Kamati ya Mapitio ya Sheria ya Elimu Sura ya 353 kwa wadau wa elimu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda amesema serikali inalenga kuhakikisha mchakato huo unakamilika ifikapo mwaka 2027.
Amesema sheria hiyo ambayo ilitungwa mwaka 1978 imekuwa ikifanyiwa marekebisho ya hapa na pale, lakini sasa ipo haja ya kufanya tathmini ya kina ili kuona kama nchi inahitaji sheria mpya kabisa au kuendelea kuboresha iliyopo.
“Baada ya uzinduzi wa sera mpya ya elimu, hatua inayofuata ni kuhakikisha sheria ya elimu inaendana na mwelekeo mpya wa sekta hii muhimu,” amesema Profesa Mkenda.
Aidha amesema serikali inalenga kupata maoni mapana kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuhakikisha sheria itakayopatikana inakuwa na tija, inazingatia mazingira ya sasa na inalinda maslahi ya taifa kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Caroline Nombo amesema wizara ipo tayari kupokea na kuyafanyia kazi maoni yote yatakayowasilishwa na wadau katika mchakato huo.
Amewasisitiza washiriki kutumia nafasi hiyo kutoa maoni ya kitaalamu yatakayosaidia kupatikana kwa sheria bora itakayochochea maendeleo ya elimu nchini.
Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir amesema ucheleweshaji wa maboresho hayo umetokana na dhamira ya serikali kuhakikisha wananchi wengi wanapata nafasi ya kushiriki kutoa maoni yao.
Amesema kutokana na mabadiliko makubwa ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia yaliyotokea tangu kutungwa kwa sheria hiyo, ipo haja ya kuwa na sheria imara na endelevu itakayokidhi mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho.



Social Plugin