Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MOIL ENERGIES YAIPONGEZA SERIKALI KWA KUDHIBITI MAKALI YA BEI YA MAFUTA NA KUTOA RUZUKU YA DIZELI

Meneja Mwekezaji wa Bohari ya Mafuta ya MOIL Energies Dkt. Sajad Habib Rai

MENEJA Mwekezaji wa Bohari ya Mafuta ya MOIL Energies Dkt. Sajad Habib Rai, amesema Serikali ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha mafuta yanaendelea kupatikana nchini huku ikidhibiti makali ya ongezeko la bei linalochochewa na mgogoro wa Mashariki ya Kati unaohusisha Iran, Israel na Marekani.

Kwa mujibu wa bei mpya za Mei 2026 zilizotangazwa na EWURA, petroli Dar es Salaam itauzwa Sh4,115 kwa lita, dizeli Sh4,248 huku mafuta ya taa yakifikia Sh4,677 kwa lita huku Serikali pia imeendelea kuingiza ruzuku ya Sh259 kwa kila lita ya dizeli hatua inayosaidia kupunguza mzigo kwa wananchi pamoja na sekta za uzalishaji.

Kwa mujibu wa Dkt. Sajad Habib Rai, Ruzuku ya Sh 259 kwa kila Lita ya Dizeli iliyowekwa na Serikali kwa kiasi fulani inasaidia kupunguza makali hasa kwa upande wa usafirishaji na usafiri wa umma ambao kwa asilimia kubwa hutumia nishati hiyo ya Dizeli.

"Tunaipongeza Serikali kwa kuweka Ruzuku hiyo, ukweli kwa kiasi fulani inasaidia kupunguza mzigo wa makali yatokanayo na kupanda kwa bei, siyo kila nchi Duniani imechukua hatua hii kwa maana hali inayojitokeza sasa ya ukata wa mafuta ni tatizo kwa Dunia nzima", amesema Dkt. Sajad.

Amesema katika ukanda wa Afrika Mashariki, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kutangaza bei mpya za mafuta kwa mwezi Mei kutokana na utaratibu wake wa kutangaza bei kila Jumatano ya kwanza ya mwezi, hali inayofanya mwenendo wa bei nchini kuwa kiashiria muhimu cha matarajio ya soko la mafuta kwa nchi jirani.

Amesisitiza kuwa Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye unafuu mkubwa wa mafuta katika ukanda huo wa Afrika Mashariki  mataifa mengine yakitarajiwa kutangaza bei mpya zenye ongezeko kubwa zaidi kutokana na presha iliyopo katika soko la dunia.

Dkt. Sajad amewashauri Watanzania wote kuendelea kuiunga Serikali mkono wakati huu ambapo inaendelea kutafuta njia zaidi za kupunguza makali hayo ya mafuta yaliyosababishwa na uwepo wa mgogo unayoendelea Mashariki ya kati.

Amesema wao kama wafanyabiashara wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma za mafuta kwa utaratibu bora zaidi na bila upendeleo kwa mtu ili kuepusha lawama zisizotarajiwa.
 
Aidha kwa mujibu wa bei za mwezi uliopita katika nchi jirani, Kenya petroli ilikuwa tayari imevuka zaidi ya Sh4,300 za Kitanzania kwa lita huku Uganda ikikaribia Sh4,500 kwa lita katika baadhi ya maeneo huku zote zikizidiwa na  nchi ya Rwanda ambayo  yenyewe ilikuwa tayari imefikia zaidi ya Sh5,200 za Kitanzania kwa lita ya petroli, hali inayoifanya kuwa miongoni mwa nchi zenye gharama kubwa zaidi za mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com