Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.
Mtatiro ametoa rai hiyo leo Mei 7, 2026 wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga, ambapo amesema kiwango cha ukusanyaji wa mapato kwa sasa kimefikia asilimia 60 na kusisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Amesema mapato ya ndani yana mchango mkubwa katika kuboresha huduma za kijamii na maendeleo ya miundombinu, hivyo watendaji pamoja na madiwani wanapaswa kushirikiana kuhakikisha vyanzo vya mapato vinasimamiwa kwa ufanisi zaidi.
“Ushirikiano ni jambo muhimu katika kuijenga halmashauri yetu. Kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha tunafikia maendeleo tunayoyahitaji,” amesema Mtatiro.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amegusia changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, akisisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali kushirikiana kumaliza tatizo hilo ili kuwawezesha watoto hao kupata mazingira bora ya malezi na elimu.
Kitumbo amesema ushirikiano baina ya madiwani na watendaji ndiyo msingi wa mafanikio ya manispaa, huku akihimiza kuongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ili kuiwezesha halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi.
Amesema changamoto zote zilizowasilishwa na madiwani zitafanyiwa kazi hatua kwa hatua, huku akitambua kuwa bado baadhi ya kata zinakabiliwa na changamoto mbalimbali za maendeleo.
Meya huyo ameongeza kuwa halmashauri itaendelea kutafuta suluhisho la changamoto hizo, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya vyoo shuleni pamoja na barabara, ili kuboresha huduma kwa wananchi wa Manispaa ya Shinyanga.
Social Plugin