Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, ambaye pia ni Mbunge wa Kondoa Mjini, Mariam Ditopile, ameipongeza Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuwawezesha vijana nchini.
Akisoma taarifa ya Kamati hiyo bungeni kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na maoni ya Kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Ditopile amesema sehemu ya fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni nne, zimeelekezwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO).
Amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali katika kukuza uchumi wa vijana kwa kuwajengea uwezo wa kujiajiri, kuanzisha biashara endelevu na kuhamasisha ubunifu katika sekta ya viwanda.
“Hatua hii ni chachu muhimu ya maendeleo ya vijana na inaendelea kuimarisha dira ya Tanzania ya kujenga uchumi shindani unaojumuisha wananchi wote, hususan vijana ambao ndio nguvu kazi kubwa ya taifa,” alisema Ditopile.
Aidha, Kamati hiyo imeeleza kuwa uwekezaji huo utaongeza fursa za ajira na kuchochea maendeleo ya sekta ya viwanda vidogo nchini.

Social Plugin