Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amezitaka taasisi za elimu ya juu nchini kuhakikisha tafiti, ubunifu pamoja na matumizi ya teknolojia vinaelekezwa katika kutoa suluhisho la changamoto halisi zinazowakabili wananchi na kuchochea maendeleo ya taifa.
Dk. Komba alisema hayo wakati akifungua Maadhimisho ya Wiki ya 11 ya Utafiti na Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kishiriki cha Elimu (DUCE), yaliyowakutanisha wanafunzi, wahadhiri, watafiti, wabunifu pamoja na wadau mbalimbali wa elimu na maendeleo.
Aidha, alieleza utayari wake wa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kishiriki cha Elimu (DUCE), Taasisi ya Global Education Link (GEL) pamoja na wadau wengine wa elimu nchini katika kuimarisha mwongozo wa taaluma kwa wanafunzi na walimu ili kuwaandaa vijana kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa na ya baadaye.
Utayari huo umeelezwa na Dkt. Komba wakati alipotembelea banda la Global Education Link katika maadhimisho hayo, ambapo alisema changamoto ya mwongozo wa taaluma imekuwa kubwa nchini huku akisisitiza kuwa maandalizi ya mwanafunzi kuhusu mustakabali wake yanapaswa kuanza mapema tangu akiwa shule ya msingi.
Alisema maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila uwekezaji mkubwa katika elimu, tafiti, ubunifu, teknolojia na ushirikishwaji wa jamii, huku akisisitiza kuwa elimu bora haipaswi kuishia darasani pekee bali iwe nyenzo ya kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
“Tafiti na ubunifu vinapaswa kuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa jamii. Tusifanye tafiti ambazo zinaishia kwenye makabati, bali tafiti zinazotoa majibu ya changamoto za wananchi,” alisema Dkt. Komba.
Alisema kuwa katika dunia ya sasa matumizi ya teknolojia na mifumo ya kidijitali ni muhimu katika kuongeza ufanisi wa kazi, kuboresha huduma kwa jamii pamoja na kuharakisha maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, uchumi, mazingira, usafiri na afya.
Dkt. Komba alisema pia kuna umuhimu mkubwa wa kuwajengea uwezo walimu waliopo mashuleni ili wawe sehemu ya mfumo wa kuwaelekeza wanafunzi katika uchaguzi sahihi wa taaluma.
“Tunapaswa kuhakikisha watoto wanaelewa mapema wanataka kufanya nini katika maisha yao. Akishafanya maamuzi yasiyo sahihi katika hatua za awali inaweza kuwa changamoto kubwa baadaye,” alisema.
Kaimu Mkuu wa DUCE, Prof. Amani Lusekelo, alisema hadi sasa jumla ya tafiti 45 zimefanyika kupitia programu ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu na baadhi yake tayari zimeanza kutumiwa na halmashauri mbalimbali nchini katika kuboresha huduma za kijamii na elimu
Prof. Lusekelo alisema maadhimisho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonesha kazi za watafiti na wabunifu pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya vyuo vikuu, serikali, sekta binafsi na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel, alisema bado kuna changamoto kubwa ya wanafunzi wengi kuchagua taaluma kwa kufuata mitazamo ya kijamii badala ya kuzingatia mahitaji halisi ya ajira na maendeleo ya dunia ya sasa.
Alisema tafiti walizozifanya katika shule mbalimbali zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi wa masomo ya sayansi, hususan PCB, wanataka kusomea udaktari huku kada nyingine muhimu zikiwa na uhaba mkubwa wa wataalamu.
“Tunawakuta wanafunzi wengi wa PCB wanataka kuwa madaktari, lakini ukiangalia mahitaji ya sasa kuna maeneo kama radiology, physiotherapy, audiology, speech therapy, dialysis na dentistry yenye uhitaji mkubwa wa wataalamu lakini wanafunzi hawapelekwi huko kwa sababu hawapati mwongozo sahihi wa taaluma,” alisema Mollel.
Kaulimbiu ya Wiki ya 11 ya Utafiti na Ubunifu DUCE mwaka huu imejikita katika matumizi bora ya rasilimali za madini nchini kwa ajili ya kuendeleza nishati jadidifu, mabadiliko ya kidijitali pamoja na kuimarisha usalama wa jamii.
Washiriki wa maadhimisho hayo pia walipata fursa ya kuonesha bunifu mbalimbali za kiteknolojia pamoja na tafiti zinazolenga kutatua changamoto zinazoikabili jamii katika sekta mbalimbali.









Social Plugin