Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UMUHIMU WA RIPOTI YA OKTOBA 29, SABABU TUME KUONGEZEWA MUDA ZAIDI



Mwenyekiti wa Tume ya uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa amani ya wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 Jaji Mstaafu Othman Chande amesema Tume hiyo imeongezewa siku zaidi za kukamilisha kazi yake kutokana na sababu za kitaalamu na umuhimu wa kutoa ripoti yenye ukweli na haki kwa wananchi.

Jaji Mstaafu Chande amebainisha hayo leo Jumatano Aprili 08, 2026 mbele ya waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam, akikanusha uvumi unaonezwa katika mitandao ya kijamii kuwa Tume hiyo imeongezewa muda wa siku 21 ili kurekebisha taarifa yake kwa kuchakachua baadhi ya taarifa.

"Tume imeongezewa muda kwa sababu nne; Moja ni ushahidi mwingi unaoendelea kuingia hivi sasa na pili ni ushauri wa kitaalamu ambao tumeomba na wataalamu wa sayansi wanaendelea kutupa, tatu ni kuchambua kwa kina ushahidi mwingi ambao tumeupata na mwisho ni kuhakikisha kwamba ripoti ikitoka inatoka kwa lugha mbili za mpigo yaani Kiingereza na Kiswahili ili kila mwananchi aelewe." Amekaririwa Jaji Mstaafu Othman Chande.

Chande amebainisha kuwa sababu hizo zipo hadharani na zimetangazwa kwenye gazeti la serikali na amewahakikishia watanzania kuwa hawapaswi kuwa na hofu kuhusu uadilifu wa ripoti hiyo, akisisitiza kuwa tume hiyo inafanya kazi kwa uhuru bila shinikizo la nje.

Tume hiyo iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan novemba 20, 2025 kuchunguza matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, imeongezewa muda mara mbili ambapo awali ilipewa siku 90 kabla ya kuongezea siku 42 na wiki hii ikaongezewa siku nyingine 21, ambapo sasa itakamilisha kazi yake April 24, 2026.

Moja ya majukumu ya tume hiyo ni kuchunguza kiini cha vurugu za uchaguzi huo zilizosababisha vifo vya watu kadhaa na uharibu mkubwa wa mali zikiwemo ofisi za umma, vituo vya mafuta na vituo vya Polisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com