Wakizungumza katika ibada na misa za Ijumaa Kuu jana maeneo mbalimbali nchini, viongozi hao walibainisha kuwa kumbukumbu ya mateso ya Yesu Kristo ni fundisho tosha kuwa ushindi na mabadiliko ya maisha huja kupitia uvumilivu na kutoacha matumaini hata katika nyakati ngumu.
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk. Abednego Keshomshahara, alihimiza jamii kupaza sauti kukataa roho za vita na chuki, akibainisha kuwa kufufuka kwa Kristo ni ishara ya matumaini mapya yanayoweza kubadili magumu kuwa heri.
Alisisitiza kuwa mwanadamu hapaswi kukata tamaa mbele ya changamoto za maisha, kwani imani thabiti ndiyo inayomvusha mtu kutoka kwenye mateso kuelekea kwenye ushindi wa kudumu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UKAMA Arusha, Askofu Dk. Stanley Hotay, alieleza kuwa Ijumaa Kuu si tukio la kihistoria tu, bali ni ujumbe hai unaopaswa kutumiwa na Watanzania kama chombo cha mabadiliko.
Alikumbusha kuwa msalaba ni chanzo cha ukombozi kinachofundisha msamaha badala ya kulipiza kisasi, akitoa mwito wa kutumia maadhimisho haya kujitathmini kitaifa ili kuondoa uhasama na kuanza upya kwa mustakabali wa nchi.
Naye Askofu wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, Stephano Musomba, aligusa kiini cha maridhiano kwa kusema kuwa taifa haliwezi kusonga mbele kwa kusifiana pekee, bali kwa kuambizana ukweli unaojenga.
Alisisitiza kuwa ukweli unaweza kuuma, lakini ndio dawa pekee itakayoliongoza taifa kuelekea kwenye umoja, wema na uzuri, huku akiwaonya waumini kuwa kutoumeza ukweli ni kutoitakia mema nchi na vizazi vijavyo.
Wito huo ulihitimishwa na Mchungaji Wilbroad Mastai wa KKKT Kimara, aliyewataka waumini kuifanya ajenda kuu ya mioyo yao kuwa ni shukrani.
Alisema kuwa katika kipindi hiki cha mwaka 2026, dhabihu ya upendo na shukrani ndiyo inayopaswa kutamalaki, ikiwa ni msingi wa kuijenga jamii yenye amani na maridhiano yanayovuka mipaka ya kidini na kijamii.

Social Plugin