Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA PAC ZANZIBAR YAVUTIWA NA MRADI WA UMEME JUA KISHAPU… YASEMA NI UWEKEZAJI MKUBWA WA KIMKAKATI

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar (PAC) wakikagua utekelezaji wa mradi wa umeme wa jua katika kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga, Wilaya ya Kishapu, walipofika eneo la mradi huo kwa lengo la kujifunza namna unavyotekelezwa na manufaa yake kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC Kombo Mwinyi Shehe akizungumza baada ya kutembelea mradi wa umeme juu kijiji cha Ngunga.
Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali Baraza la wawakilishi Zanzibar (PAC), imetembelea mradi wa umeme jua wa Kishapu Mkoani Shinyanga ili kujifunza namna mradi huo unavyotekelezwa.

Ziara hiyo imefanyika leo Aprili 2, 2026, ambapo wajumbe wa kamati wameridhishwa na namna mradi huo unavyotekelezwa huku wakipongeza uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika kuhakikisha changamoto ya umeme inakwisha nchini.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Kombo Mwinyi Shehe amesema hali ya umeme Zanzibar si ya kuridhisha na kuomba Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuongeza kiwango cha umeme kinachouzwa visiwani humo ili kukabiliana na upungufu uliopo.

“Mahitaji ya umeme yanaongezeka lakini umeme uliopo haukidhi mahitaji tunawasilisha ombi letu kwa TANESCO ituongezee kiwango cha umeme kwa kuwa sisi ni wateja wazuri na hatuna deni” amesema Shehe.

Amesema ujio wa kamati hiyo Kishapu ni sehemu ya juhudi za kutafuta mbinu mbadala hususan matumizi ya nishati mbadala kama umeme wa jua, ambao umeonekana kuwa na mafanikio bila kuathiri shughuli za kijamii na mazingira.

Amesema watakwenda kutoa ushauri kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuona kama kuna uwezekano wa kuwekeza mradi mkubwa kama wa Ngunga ambao utasaidia kupunguza changamoto ya umeme kutokana na shughuli nyingi za uwekezaji kuongezeka na mahitaji kuwa makubwa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Timothy Mgaya akifafanua juu ya utekelezaji wa mradi wa umeme jua.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Timothy Mgaya, amesema tayari kuna juhudi zinazoendelea kuongeza upatikanaji wa umeme Zanzibar, ikiwemo utekelezaji wa mradi wa kebo ya chini ya bahari (submarine cable) unaounganisha visiwa vya Unguja na Mafia.

Amesema TANESCO imekuwa ikiruhusu sekta binafsi kushiriki katika uwekezaji wa miradi ya umeme jua katika maeneo mbalimbali yenye kiwango kikubwa cha jua kama Dodoma, Manyara na Same ili kuongeza uzalishaji wa umeme.
Mwenyekiti wa Kamati ya PAC Kombo Mwinyi Shehe akizungumza baada ya kutembelea mradi wa umeme juu kijiji cha Ngunga.
Mjumbe wa kamati ya PAC Mohamed Manzi Haji

Mjumbe wa kamati hiyo na Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira Zanzibar, Mohammed Manzi Haji, amesema wanahitaji kujifunza kwa kina namna miradi hiyo inavyotekelezwa kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira ili waweze kutumia uzoefu huo katika mipango yao.
Mjumbe wa Kamati ya PAC Salma Mussa Bilal





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com