Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Bagamoyo, Mkoani Pwani Baba Askofu Stephano Lameck Musomba, amelaani vikali tabia ya baadhi ya wananchi kushangilia vifo vya viongozi, akisema kitendo hicho ni ishara ya mmomonyoko wa maadili katika jamii, akipendekeza mazungumzo na majadiliano zaidi katika kuondoa changamoto na tofauti za kisiasa na kijamii zilizopo nchini.
Akihubiri wakati wa Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika Aprili 3, 2026 katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima wa Karmeli, Bunju, Mkoani Dar Es Salaa, Baba Askofu Musomba amesema hali hiyo inaonesha kuwa kuna tatizo kubwa la kijamii linalohitaji kutazamwa kwa kina na ukweli kuwekwa wazi ili kupata suluhisho la kudumu.
Amesema kuwa katika mila za Kiafrika, kifo hakikuwa tukio la kushangiliwa bali ni wakati wa huzuni na mshikamano, akiongeza kusema kuwa mabadiliko hayo ya kitabia yanaashiria kupotea kwa misingi ya utu na maadili ya jamii, suala ambalo halipaswi kuvumiliwa na kuonekana kama jambo la kawaida.
“Si kawaida kwa jamii yetu kushangilia kifo, tulizoea kuomboleza na kuungana katika huzuni, lakini sasa hali imebadilika na inapaswa kututia wasiwasi,” amesema Baba Askofu.
Aidha Askofu Musomba ametoa wito kwa wananchi kuelimishana, kuvumiliana na kutafuta haki kwa njia sahihi, akionya kuwa bila kufanya hivyo jamii inaweza kuendelea kupoteza mwelekeo na kuingia katika migogoro isiyo ya lazima, akitahadharisha pia kuongezeka kwa imani za kishirikina katika jamii nyingi nchini.
Katika mahubiri yake ya Ijumaa Kuu, Askofu Musomba pia ametahadharisha waumini wa Kanisa Katoliki na Watanzanka kwa ujumla kuhusu kuongezeka kwa tabia na imani za kishirikina katika jamii, akisema suala hilo ikiwa litaendelea kuvumiliwa na kuonekana kuwa la kawaida litasababisha madhara makubwa kwa jamii kwa siku za mbeleni.

Social Plugin