
Na Paschazia Charles - Shinyanga
Utolewaji wa chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa polio kwa awamu ya kwanza unatarajiwa kuanza tarehe 24 Machi 2026 na kuhitimishwa tarehe 27 Machi 2026 mkoani Shinyanga, ambapo jumla ya watoto 781,166 wanatarajiwa kufikiwa.
Akizungumza katika kikao kazi cha kamati ya afya kuhusu kampeni ya chanjo ya polio kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa afya na kufanyika katika ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Yudas Lucas Ndungile, amesema chanjo hiyo itatolewa bure kwa watoto chini ya umri wa miaka kumi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani, shuleni na katika vituo maalumu vilivyowekwa.
“Zoezi litaanza tarehe 24 na itamalizika tarehe 27 mwezi wa tatu 2026, zoezi hili limekuja kutokana na umuhimu wa uwepo wa viashiria vya vimelea vya ugonjwa wa polio vilivyobainika katika maji taka mkoani Mwanza hivyo kuilazimu Serikali kuja na mpango mkakati wa kuwakinga watoto chini ya miaka kumi kwa mikoa saba,” amesema Dkt. Ndungile.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamdun, akifungua kikao hicho, amewataka wazazi wa watoto chini ya umri wa miaka 10 kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo hiyo ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa polio.
“Nitoe wito kwa wananchi na wakazi wote wa mkoa wa Shinyanga kuruhusu watoto wote kupatiwa chanjo tumethibitisha na tumedhibitishiwa kwamba chanjo hii ni salama kwa hiyo tuhakikishe kwamba wazazi, walezi, walimu na wahamasishaji wote wananshiriki kutoa elimu na kuruhusu watoto waweze kupatiwa chanjo ili kuweze kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza,” amesema Hamduni.
Naye mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambaye pia ni Mratibu wa miradi ya afya ya uzazi na mtoto, Bi. Dinah Atonda, amesema maandalizi yote ya zoezi hilo yamekamilika, ikiwemo upatikanaji wa vifaa pamoja na mikakati ya kuyafikia makundi mbalimbali.
“Tunawaomba kamati hii ambayo ni muhimu sana kusimamia zoezi hili ili tufanikiwe na tuweze kufikia malengo ya kuchanja watoto 781,166 kama ambavyo Mganga Mkuu ametangulia kusema,” amesema Atonda.
Kwa upande wake, Mratibu wa chanjo Mkoa wa Shinyanga, Timoth Sosoma, amesema chanjo hiyo ni muhimu kwa kuwa itasaidia kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa wa polio, hasa baada ya kugundulika kwa kimelea cha ugonjwa huo kwenye maji taka mkoani Mwanza.
Chanjo hiyo itatolewa kwa watoto chini ya umri wa miaka kumi katika mikoa saba ambayo ni Geita, Tabora, Mwanza, Simiyu, Mara, Singida na Shinyanga, ikiwa na kaulimbiu isemayo: “Mpe chanjo mtoto wako, linda tabasamu la mtoto, zuia polio.”









Social Plugin