Na mwandishi Maalum, Malunde Blog Dodoma.
Zaidi ya Watanzania milioni sita wanatarajiwa kunufaika na mpango wa Go Green na Imbeju, unaotekelezwa na CRDB Bank Foundation chini ya CRDB Benki, kwa lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi huku ukilinda mazingira.
Mpango huo ambao umezinduliwa rasmi Februari 12, 2026 jijini Dodoma ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ni uwekezaji wa zaidi ya shilingi milioni 500 na unaanza kutekelezwa kabla ya kuanza rasmi kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2026.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Dkt.Kitila amesema hatua hiyo inaonesha namna sekta binafsi inavyoitikia kwa vitendo vipaumbele vya Serikali, hususan katika kurasimisha biashara ndogo ndogo na kukuza uchumi wa wananchi.
Amesema mpango wa Go Green na Imbeju unalenga kugusa maeneo nyeti ya maendeleo kwa kuwapa vijana na makundi mengine fursa za kiuchumi zitakazochochea ajira, kipato na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, huku ukiwa na mchango wa moja kwa moja katika kulinda rasilimali za Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa CRDB Benki, Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo imetoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo licha ya kuwepo kwa wadau wengine.
Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, shilingi milioni 10 zitatumika kuwajengea uwezo wa teknolojia wanufaika, milioni 10 ni dhamana kwa wajasiriamali wasiojiweza, milioni 10 nyingine kwa ajili ya sera na mifumo ya utekelezaji, huku kiasi kilichobaki kikitengwa kama ruzuku ya kusaidia miradi kuanza na kukua kwa uendelevu.
Kutokana na hayo Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, Oswald Urassa, amesema taasisi hiyo imejikita kuwekeza kwa vijana kwa kuwatambua kama rasilimali muhimu ya Taifa, akibainisha kuwa idadi kubwa ya Watanzania ni vijana wanaohitaji maarifa, mitaji na fursa ili kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya nchi.
Amesema kupitia mpango huo, vijana wanapatiwa mafunzo ya ujasiriamali yanayowawezesha kutambua na kutumia fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta za umma na binafsi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Ester Mwambapa, amesema katika utekelezaji wa kipengele cha Imbeju, taasisi hiyo imeingia makubaliano na vyuo vikuu 18 vya elimu ya juu pamoja na vyuo vya ufundi vikiwemo SIDO na VETA, kwa lengo la kuwawezesha wahitimu kuingia katika shughuli za uzalishaji na biashara endelevu.
Amesema hadi sasa wanufaika 1,275 tayari wamepata fursa kupitia mpango huo, huku baadhi yao wakianza miradi inayochangia ajira, kipato na uhifadhi wa mazingira.
Mpango wa Go Green na Imbeju unatajwa kuwa miongoni mwa mikakati muhimu ya kuunganisha ajenda ya mazingira, uwezeshaji wa vijana na maendeleo jumuishi ya Taifa, huku ukitarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi kwa maelfu ya vijana na wajasiriamali nchini.




Social Plugin