Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chan’ga akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2026 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka, ikieleza kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chan’ga, alisema mvua hizo zinatarajiwa zaidi katika Pwani ya Kaskazini pamoja na baadhi ya maeneo ya Kanda ya Ziwa Viktoria, hususan mikoa ya Kagera na Geita.
Dkt. Chan’ga alibainisha kuwa maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na baadhi ya mikoa ya Ziwa Viktoria ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
Kwa mujibu wa TMA, mvua za Masika zinatarajiwa kuanza mwishoni mwa Februari hadi Machi 2026, huku zikiisha kati ya Mei na Juni 2026, na ongezeko la mvua likitarajiwa zaidi mwezi Aprili.
Alisema athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na mafuriko, kujaa kwa mito na mabwawa pamoja na kuathirika kwa mazao katika maeneo yatakayopata mvua nyingi, huku maeneo yenye mvua chache yakikabiliwa na upungufu wa maji.
TMA imewataka wananchi na wadau kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa na kuzingatia ushauri unaotolewa ili kujikinga na madhara ya matukio ya hali mbaya ya hewa.










Social Plugin