Na Josephine Manaseh,Dodoma
MRATIBU wa Mtandao wa Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi Tanzania (GCCTC), Maria Matui, amesema hakuna kundi litakaloachwa nyuma ikiwa kutakuwa na ushirikishwaji wa kutosha kwa vijana wa kike na wa kiume, pamoja na watu wenye ulemavu, kwa kuzingatia usawa na ujumuishi.
Matui alieleza hayo juzi wakati wa mkutano wa mwongozo wa majadiliano na wadau wakuu pamoja na wizara za kisekta, ulioandaliwa na GCCTC kwa kushirikiana na Shirika lisilo la kiserikali la Women Action Towards Economic Development (WATED) Tanzania.
Wizara zilizoshiriki majadiliano hayo ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Katiba na Sheria, pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Alisema kuwa mwongozo wa majadiliano unalenga kuhakikisha kuwa hakuna kundi linaloachwa nyuma, na kila kundi linapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika michakato ya maamuzi na utekelezaji.
Aidha, mwongozo unatambua hitaji la dharura la kuimarisha ushiriki, sauti, na ushawishi wa wanawake na vijana katika majadiliano ya tabianchi.
Matui alisema kuwa Tanzania kwa sasa inaendeleza michakato muhimu ya tabianchi, ikiwemo utekelezaji wa Michango Iliyoamuliwa Kitaifa (NDCs), mifumo ya fedha za tabianchi, mikakati ya adaptation na mitigation, pamoja na ushiriki katika majadiliano ya kikanda na kimataifa.
Hata hivyo, alibainisha kuwa licha ya kuwepo kwa ahadi za usawa wa kijinsia na ujumuishaji wa vijana, ushiriki wa maana wa wanawake na vijana bado ni mdogo.
“Mashauriano na wadau yalibainisha mapengo katika upatikanaji wa maarifa, mwongozo wa vitendo, na uratibu, hasa kwa wanawake wa ngazi ya jamii, vijana, na wadau wa asasi za kiraia,” alisema.
Aliongeza kuwa kuna uhitaji mkubwa wa mwongozo unaorahisisha uelewa wa majadiliano ya tabianchi, unaofafanua namna ya kushiriki na kuwapa wanawake na vijana zana za kushiriki kwa ujasiri na kwa mkakati.
Mwongozo huu utasaidia kuunda uwezo, kuimarisha uratibu kati ya serikali na wadau wasio wa kiserikali, na kuchangia maamuzi ya tabianchi yanayojumuisha usawa wa kijinsia na kushirikisha vijana.
“Mpango huu unaendana na sera za kitaifa za jinsia na vijana, ahadi za Tanzania kuhusu mabadiliko ya tabianchi, huku ukihakikisha kuwa wanawake na vijana hawapo tu kwenye meza ya maamuzi, bali wana ushawishi wa kweli katika kuunda matokeo ya tabianchi yanayoathiri maisha yao na vizazi vijavyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Tree of Hope ya Mkoani Tanga, Fortunata Manyeresa, amesema mwongozo huo unalenga kujengea uwezo wataalam, kupata maoni kutoka kwa wadau, na kutoa mafunzo elekezi ya namna ya kushiriki vikao vya majadiliano ya tabianchi kimataifa. “Mwongozo umeelekezwa kwa makundi mbalimbali ya wanawake, ikiwemo wa vijijini na mijini,” alisema.

Social Plugin