Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MEYA IRANQHE AHIMIZA MAANDALIZI YA AFCON 2027 ARUSHA


Na Bora Mustafa, Arusha.

Katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka, Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Iranqhe, ametia uamsho wa kuweka mikakati madhubuti ya maandalizi kuelekea mashindano ya AFCON 2027.

Amesema kuwa katika nchi jirani za Afrika Mashariki tayari mabango ya kukaribisha mashindano hayo yameanza kuwekwa, tofauti na ilivyo nchini hususan katika Jiji la Arusha ambalo linatarajiwa kuwa mwenyeji wa ugeni huo.

Aidha, Iranqhe amelitaarifu baraza hilo kuwa jiji limejipanga kujiendesha kwa mapato ya ndani bila kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu. Amesema uchumi wa halmashauri unaweza kufanikisha azma hiyo kwa kuiga mfano wa nchi ya China, ambayo imefanikiwa kwa kuwekeza katika serikali za mitaa.

“Huu ni wakati muafaka wa kuboresha eneo la stendi ndogo. Eneo hilo litaboreshwa bila kuwabugudhi wafanyabiashara waliopo. Sambamba na hayo, uwekezaji katika masoko yetu unatakiwa kufanyika. Hii yote ni kupandisha hadhi ya jiji, kuangalia uwekezaji wa kiwanda cha nyama cha Arusha Meat, pamoja na kutoa mikopo kwa watu wenye ulemavu, wanawake na vijana. Hatua hizi zikikamilika, mapato ya serikali yataongezeka,” amesema Iranqhe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, amewataka madiwani kudumisha ushirikiano, uwajibikaji na nidhamu kazini. Pia amesisitiza umuhimu wa kufuata misingi ya kazi na kuwasikiliza wananchi badala ya kuwavunja moyo.

Vilevile, ametoa rai kwa watendaji wanaowakwamisha wananchi wanaoomba mikopo ya halmashauri, akisema fedha zimekuwa zikibaki katika mfuko wa maendeleo ya jamii jambo ambalo ni kinyume na utaratibu na linarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Hata hivyo, Mkude amesema kuna masuala mbalimbali yanayopaswa kuangaliwa upya, ikiwemo kukithiri kwa adhabu mashuleni, hamasa ya kujiunga na bima ya afya kwa wote, wazazi kutotozwa michango isiyo halali pamoja na kupambana na matumizi ya rushwa.

“Kipindi hiki kila mmoja ni shahidi wa mabadiliko ya tabia ya nchi, wahimizeni wananchi kutunza chakula,” amesema Mkude.

Katika namna hiyohiyo, Diwani wa Kata ya Unga Limited, Mahmoud Said, akichangia hoja yake ameomba kuwekwa matuta katika barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 1.8 ili kuwalinda wanafunzi dhidi ya ajali zinazoweza kujitokeza.












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com