Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWALIMU NA MWENZAKE WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA TUHUMA ZA MAUAJI YA MKE WA MENEJA TARURA

 

Na Mwandishi Wetu, Musoma

MWALIMU anayefundisha shule binafsi ya msingi na Sekondari Mbalali, mkoani Mbeya , Marco Marco Maginga mwenye umri wa miaka 47 na Mwita Abel Maginga (45) mkazi wa wilayani Tarime, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na shtaka la mauaji ya Rodha Jonathani (42) mkazi wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Washtakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Musoma, Eligeria Rujwahuka ambapo wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 196 na kifungu cha 197 cha kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba , 23, 2025 kwa kumuua Rhoda Jonathan Mobe mkazi wa Kijiji cha Burunga , Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti.

Kwa upande wa mashitaka, wakili wa serikali Joyce Matindwa, amesema kwamba shauri lililokuja kwa ajili ya kutajwa hali ya upelelezi bado haujakamilika.

Wakili Joyce ameiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya shauri hilo kutajwa.

Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, Eligenia Rujwahuka amesema shauri hilo halina dhamana na mahakama hiyo haina mamlaka zaidi ya kusubili taratibu za upelelezi.

Wakili Linus Amri anayewakilisha wanafamilia na Ndugu wa marehemu ambaye yupo kwa ajili ya kuangalia mwenendo wa kesi hiyo amesema tayali watuhumiwa wamefikishwa mahakamani lakini bado Jamhuri haijakamilisha upelelezi.

Anapendekeza upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi" wakamilishe upelelezi kwasababu ni kesi ambayo imeamsha hisia za watu kutokana na tukio la kikatili alilotendewa Rhoda ambaye kwa sasa ni marehemu baada ya kuaawa nyumbani kwake kwa kukatwa katwa mapanga.

Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Januari, 5, 2026 itakapotajwa tena na washtakiwa wamerudishwa rumande. Wakili wa washtakiwa hao wawili ni Mluge Karol .

Awali Oktoba , 26, 2025 Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara, Pius Lutumo, alisema kuwa Jeshi la Polisi mkoa wa Mara linamshikilia Wilson Mwita Charles mwenye umri wa miaka 52 mkazi wa Kitongoji cha Burunga , Kata ya Uwanja wa Ndege wilayani Serengeti na watu kadhaa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Rhoda Jonathani .

Kamanda Pius alisema kuwa baada ya uchunguzi wa awali Jeshi la Polisi mkoani humu linamshikilia Wilson Mwita Charles ambaye ni mume wa marehemu kwa ajili ya mahojiano zaidi ya tukio hilo. Waliofikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na shtaka la mauaji ni Mwita Abel na Marco Marco.

Familia ya marehemu akiwemo mama mzazi Ester Mobe ameiangukia Serikali akiomba kutenda haki ili waliohusika kifo cha mwanae wachukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa watu wengine nia ovu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com