VIGOGO WA HALOTEL NA ZANTEL WATUPWA MAHABUSU

Watu sita wakiwamo wakurugenzi watendaji wa Kampuni za Simu za Mkononi, Le Van Dai (35) wa Halotel na Sherif El-Barary wa Zantel, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.


Makosa yao yanahusisha kula njama, kuingiza, kufunga mitambo, matumizi ya laini za simu bila usajili wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni moja.


Washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi, Calvin Mhina, anayesikiliza usikilizwaji wa awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.


Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga akisaidiana na Wakili wa Serikali, Jaqline Nyantori.


Nyantori aliwataja washtakiwa wengine ni Lei Cao maarufu kama Peter (28), Huang Yu Meng (27), Msimamizi wa Biashara wa Halotel Zanzibar, Jimmy Mosha (26), Meneja Masoko Halotel, Willy Ndoni (29), Kampuni ya Viettel Tanzania Ltd maarufu kama Halotel iliyopo Kinondoni, na Kampuni ya ZanzibarTelecomunication PLC maarufu kama Zantel ilioyopo Msasani, jijini Dar es Salaam.


Alidai katika shtaka la kwanza, kati ya Januari Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu nchini Tanzania, mshtakiwa wa kwanza hadi wa sita, walikula njama ya kutenda kosa la kutumia huduma za mawasiliano kwa njia ya udanganyifu.


Shtaka la pili, katika ya Mei Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu katika jengo la Spring lililopo Mbezi, mshtakiwa wa kwanza hadi wa sita, kwa pamoja walifunga mitambo ya mawasiliano kwa njia ya udanganyifu na kujipatia huduma za mtandao wa Halotel na Zantel bila kibali cha TCRA .


Shtaka la tatu, nne, tano na sita kati ya Januari Mosi na Desemba 31, 2017, Aprili 30,mwaka huu jijini Dar es Salaam, mshtakiwa wa tatu na wa nne, waliingiza nchini, waliifunga na kuendesha mitambo ya mawasiliano kwa kuunganisha na kampuni hizo za simu bila kibali cha TCRA.


Shtaka la nane, kati ya Mei Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu katika jengo la Spring City, mshtakiwa wa tatu na wanne, walikutwa wakitumia laini za simu za mkononi zisizosajiliwa na TCRA 281,272 za Halotel na 11,920 za Zantel.


Aidha, upande wa Jamhuri ulidai katika shtaka la 10 kati ya Mei, 2017 na Aprili 30, mwaka huu katika matawi ya Zantel ya jijini Dar es Salaam, mshtakiwa wa pili na wa nane walitumia kwa makusudi laini za simu 11,920 zisizokuwa na usajiliwa TCRA.


Shtaka la 11 na 12, kati ya Mei Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu, washtakiwa waliisababishia serikali hasara ya Sh. 1,131,936,400.


Kwa mujibu wa mashtaka yanayowakabili washtakiwa, kisheria hawakutakiwa kujibu chochote hadi upelelezi utakapokamilika itasilizwa Mahakama Kuu Tanzania, Divisheni ya Uhujumu Uchumi au kwa kibali maalumu kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).


Hakimu Mhina alisema kesi hiyo itatajwa Juni 20, mwaka huu na washtakiwa watakwenda mahabusu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527