SERIKALI YAMKABA SHINGO DANGOTE





Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ametoa siku 14 kwa uongozi wa kiwanda cha saruji cha Dangote mkoa wa Mtwara kuingia mkataba na wachimbaji wadogo wa gypsum.

Biteko ametoa kauli hiyo leo Januari 21, 2018 baada ya kutembelea kiwanda hicho na kuzungumza na viongozi wake.

Amesema mikataba hiyo inapaswa kuwa na kipengele cha kuwalipa ndani ya siku 30 baada ya kiwanda kukusanya gypsum kutoka kwa wachimbaji hao, lengo likiwa ni kuleta ufanisi na tija katika biashara zao.

“Nimekubaliana hapa kamishna wa kanda atasimamia hili la mikataba kati ya kiwanda na wachimbaji wa gypsum. Sehemu ya malipo itakuwa ndani ya mkataba na watalipa ndani ya siku 30,” amesema.

Amesema wachimbaji hao wamekuwa wakilalamikia kucheleweshewa malipo yao baada ya kupeleka kiwandani bidhaa zao.

“Nimeambiwa wachimbaji hawa walikuwa wanalipwa baada ya miezi mitatu lakini kwa mkataba huu ambao wataingia na kiwanda sasa watakuwa wanalipwa ndani ya siku 30,” amesema Biteko.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kuwasaidia wachimbaji wadogo sambamba na wawekezaji ambao wanapaswa kufanya kazi bila kusumbuliwa.

“Uwepo wa kiwanda hiki unawasaidia wachimbaji wetu waweze kupata bei nzuri pamoja na kupata soko la uhakika la kuuza bidhaa zao. Dangonte wameniahidi kwamba ndani ya muda mfupi watatekeleza agizo hili,” amesema.

Biteko amesema lengo la ziara yake ni kuwasaidia wachimbaji wa gypsum ambao hawana mikataba na kujikuta wakibanwa katika uuzaji wa bidhaa zao.
Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527