MBUNGE WA KASULU KUZUNGUKIA VIJIJI KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI


Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini Agaustine Vuma ameahidi kuzunguka vijijini kuangalia changamoto zinazowakabili Wananchi na aweze kuzifikisha Serikali zitatuliwe na wananchi waendelee kufurahia uongozi wao uliopo madarakani.

Mbunge huyo ametoa ahadi hiyo jana wakati akikagua miradi inayotekelezwa katika jimbo hilo ikiwemo mradi wa kituo cha afya cha Nyakitonto kilichotengewa kiasi cha shilingi milioni 500 ambapo mpaka sasa ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 70 mpaka sasa na fedha zilizotumika ni shilingi milioni 290.

Alisema serikali ya awamu ya tano ipo kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi na ndio maana rais Magufuli ameanza kuboresha sekta za afya kwa kutoa fedha katika vituo vya afya kwaajili ya kuwawekea wananchi huduma za afya vizuri pamoja na kuwawezesha wananchi kuwa na afya njema.

"Tunamshukuru sana rais wetu kwa kuendelea kuwasaidia Wananchi sisi kama wawakilishi wa wananchi kazi yetu ni kuibua matatizo na kumpelekea aweze kuyatatua, mpaka sasa tunaendelea kuboresha huduma za afya na nimeahidiwa kupewa fedha zingine kwa ajili ya kituo cha afya Rusesa na fedha hizo zitaendelea kutolewa kwa kuwa ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi", alisema Vuma.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu vijijini ambaye pia ni diwani wa kata ya Nyakitonto , Yohana Mshita alisema wananchi wa vijiji vilivyo karibu na kata hiyo walikuwa wakiteseka sana kupata huduma na wengine walikuwa wakilazimika kufuata huduma Kasulu mjini na kupelekea kupoteza nguvu kazi lakini kwa sasa wataendelea kupata huduma karibu.

Alisema fedha zilizotolewa zimetumika kujenga chumba cha upasuaji, wodi za wagonjwa, nyumba ya mganga na chumba cha kuhifadhia maiti, mpaka sasa kuna fedha nyingi zimebaki, na wataendelea kuzihifadhi fedha hizo na ziweze kutumika katika miradi mingine itakayoibuliwa.

Nao baadhi ya wananchi, Happynes Dastan alisema wamekuwa wakililia kupata kituo cha afya karibu kwani walikuwa wakilazimika kufuata huduma za upasuaji wilaya ya Kasulu lakini kwa sasa wana uhakika wa kupata huduma na kuendelea kufurahia huduma hiyo kwa karibu.

Alisema wanampongeza sana rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya na shughuli ya kuwahudumia wananchi wanyonge kwa shida walizokuwa nazo.
Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog Kigoma
Mbunge wa Jimbo la Kasulu Vijijini Agaustine Vuma akisalimiana na wananchi





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527