ASKOFU MKUU WA KANISA LA EAGT ATUMBULIWA...MHASIBU MKUU NAYE APITIWA



Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Evangelistic Assemblies Of God Tanzania (EAGT) imemsimamisha Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Mchungaji Brown Mwakipesile ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Wengine waliosimamishwa leo Desemba 18 ni Katibu Mkuu, Mchungaji Leonard Mwizarubi na Mhasibu Mkuu, Mchungaji PrayGod Mngonja.


Pamoja na mabadiliko hayo, bodi imewateua kwa muda kushika nafasi hizo, Askofu Mkuu atakuwa ni Mchungaji Asumwisye Mwaisabila, Katibu Mkuu atakuwa Dk Jakob Madaha na Mhasibu Mkuu atakuwa Andrea Salu.


Kwa mujibu wa Katiba ya EAGT ya Mwaka 2011 ,ibara ya 6(b)(5) kinatoa mamlaka Kwa Wajumbe wanne wa bodi hiyo kusimamisha viongozi wakuu wa kanisa akiwamo Askofu Mkuu kabla ya Mkutano Mkuu kujadili maazimio hayo.


"Baada ya siku 30 kuanzia leo  tutakuwa na mkutano mkuu wa Kanisa kwa ajili ya kupitisha mabadiliko hayo, wamesimamishwa kwa kumfukuza Makamu Askofu Mkuu wakidai alitenda dhambi, walimfukuza uchungaji na uumini pia," ni kauli ya Mwenyekiti wa bodi hiyo, John Mfuko alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Mzee Mfuko ambaye anazungumza kwa taabu kutokana na umri wake alisema kosa la viongozi hao wa kanisa ni kumfukuza bila kushirikisha bodi ya Wadhamini.

Mzee Mfuko aliyeongozana na wajumbe wawili kati ya wanne wa bodi hiyo alisema licha ya mahakama kubatilisha suala la kumfukuza, Askofu Mkuu (aliyefukuzwa) alikataa kumrejesha kanisani. Tuhuma nyingine ni kushiriki njama za kuhujumu mali za kanisa.

Baada ya kutafutwa kwa simu yake ya mkononi, Askofu aliyesimamishwa Mwakipesile hakupatikana kwenye simu yake ya mkononi.

Mbali na tuhuma hizo, bodi imewataka waumini wa kanisa hilo kutotuma pesa katika akaunti za kanisa huku ikiweka wazi kushikilia akaunti hizo kutoka mikononi mwa viongozi waliokuwa na dhamana ili kuhakiki wa mali za kanisa.

Na Kelvin Matandiko Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527