ZITTO KABWE KUFUNGUA KESI YA KIKATIBA DHIDI YA JESHI LA POLISI KWA KUSHIKILIA SIMU YAKE

Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe, amesema anajipanga kulifungulia kesi ya kikatiba jeshi la polisi nchini kutokana na kushikilia simu yake.


Zitto ameeleza kuwa simu yake inashikiliwa tangu Novemba 7 mwaka huu alipokamatwa kwa tuhuma za kuvunja sheria ya takwimu na sheria ya makosa ya mtandao.


“Walisema watahitaji simu hiyo kwa siku mbili tu, nilikwenda polisi KAMATA siku tatu baadaye nikaelezwa kuwa bado wanaendelea na uchunguzi. Nimerudi leo tarehe 20, Polisi wanasema bado wanahitaji simu yangu hiyo”, amesema Zitto.


==>Aliyoyasema Zitto kupitia akaunti yake ya Facebook:
Ndugu, Jamaa na Marafiki, mtakumbuka kuwa mnamo tarehe 7/11/2017 Jeshi la Polisi walichukua Simu yangu kwa ajili ya uchunguzi wao kuhusu tuhuma dhidi yangu kwa mujibu wa sheria ya takwimu na sheria ya makosa ya mtandao. Walisema watahitaji simu hiyo kwa siku 2 tu.


Nilikwenda polisi KAMATA siku 3 baadaye nikaelezwa kuwa bado wanaendelea na uchunguzi. Nimerudi leo tarehe 20/11/2017, Polisi wanasema bado wanahitaji simu yangu hiyo.


1) Nawakumbusha kuwa msitumie simu ile 0767777797 kwani bado imeshikiliwa na Polisi


2) Katiba ya Nchi yetu kifungu cha 16(1) na (2) imeweka msingi wa nguvu sana haki ya FARAGHA kwa raia na kwamba hata sheria ikitaka haipaswi kuingilia mawasiliano binafsi ya Raia.


Nina mashaka kuwa Jeshi la Polisi linakaa na Simu yangu muda wote huu kwa sababu za zaidi ya uchunguzi wao wa makosa wanayonituhumu nayo. Nimeamua kuwaachia Simu mpaka hapo watakapotosheka lakini wajiandae na kesi ya kikatiba ambayo pia italinda haki za wananchi wengi wanaothirika na matumizi mabaya ya sheria ya Mtandao ( cybercrime act ).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527