TAKUKURU YAWAHOJI MADIWANI WALIOJIUZULU CHADEMA

Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam, wamewahoji kwa zaidi ya saa sita, madiwani waliojiuzulu Chadema wanaotuhumiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari kuwa walipewa rushwa.

Waliofika Takukuru ni Catherine Mtui, aliyekuwa diwani wa viti maalumu, Japhet Jackson (aliyekuwa diwani wa Ambuleni) na Bryson Isangya (aliyekuwa diwani wa Maroroni). Baada ya kuhojiwa hawakutaka kuzungumza chochote wakisema wanaacha uchunguzi uendelee.

Pamoja nao, diwani wa Mbuguni, Ahimidiwe Rico anayedaiwa kuwa ndiye alirekodi sauti na picha wakati akishawishiwa na viongozi wa Serikali na wa Halmashauri ya Meru amehojiwa kwa zaidi ya saa tatu jana Jumanne Oktoba 17, 2017.

Rico amesema amewaeleza Takukuru kila kitu ambacho anakifahamu katika sakata hilo, ikiwemo kuwarekodi viongozi ambao walimshawishi kujiuzuru udiwani.

"Msimamo wangu ni kwamba, nachukia rushwa. Nimewaeleza kila kitu na wao waliniuliza kuhusu vifaa nilivyotumia kuwarekodi nikawaambia ni mali ya mbunge, alivitoa nchini Uingereza," alisema.

Rico aliyesindikizwa na diwani wa Nkwanankore, Wilson Nanyaro amesema ana imani na Takukuru kwamba watafanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua.

"Nimewaeleza wazi kuwa hata shauri hili likienda mahakamani nipo tayari kwenda kutoa ushahidi na kuthibitisha sauti za watu ambao niliwarekodi," alisema.

Alisema baada ya mahojiano yaliyoanza saa tatu hadi saa sita mchana, maofisa wa Takukuru walimwambia aondoke na watamuita watakapomuhitaji.

Hakuna ofisa wa Takukuru aliyekuwa tayari kuzungumzia mahojiano hao wakisema wasemaji ni makao makuu ya ofisi hiyo Dar yaliyoko jijini Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527