MFUNGWA ALIYEHUKUMIWA JELA MIAKA 63 KWA KUBAKA MZUNGU APIGWA RISASI NA POLISI KWENYE MAKALIO




Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Julius Mjengi akifafanua jambo wakati akitoa taarifa ya mfungwa aliyepigwa risasi wakati akitoroka mahakamani baada ya kufungwa miaka 63 kwa makosa matatu likiwemo kumbaka raia wa  Kijerumani ,kumfanyia unyang'anyi wa kutumia silaha na kumpora simu aina ya Iphone 4
............................................................................................................
Na MatukiodaimaBlog 


MFUNGWA aliyehukumiwa miaka 63 jela kwa kosa la kumbaka binti mmoja raia wa Kijerumani Gangilonga mjini Iringa Rashid Salufu (23) amejeruhiwa kwa kupigwa risasi za miguuni na makalioni wakati akijaribu kuwakimbia polisi kukwepa kutumikia kifungo hicho jela.


Imeelezwa kuwa mfungwa huyo mara baada ya kusomewa hukumu yake katika mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Iringa alipinga adhabu hiyo mbele ya hakimu kuwa hataweza kutumikia kifungu hicho kwa madai kuwa ni miaka mingi sana.


Kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Julius Mjengi alimweleza mwandishi wa matukiodaimaBlog leo ofisini kwake kuwa tukio hilo lilitokea Mei 30 majira ya saa 5 asubuhi mwaka huu katika viwanja vya makakama ya mkoa wa Iringa jengo la mahakama kuu eneo la Gangilonga mjini Iringa .


Alisema mfungwa huyo Salufi ambaye ni mkazi wa Frelimo katika Manispaa ya Iringa alikuwa na kesi CC namba 20/2017 ya kumbaka binti huyo wa Kijerumani (jina limehifadhiwa) mkazi wa Gangilonga Januari 19 mwaka huu wakati binti huyo akielekea nyumbani kwake Gangilonga na baada ya ubakaji huo alimnyang'anya simu yake na kumtishia maisha kisha kumpora simu yake aina ya Iphone 4


Aidha alisema kijana huyo alikamatwa akiwa na simu hiyo na kukiri kosa la kubaka na unyang'anyi wa kutumia silaha na kumjeruhi binti huyo hivyo kufikishwa mahakamani kwa makosa matatu na  mahakama hiyo ilimfunga miaka 30 kwa kosa la ubakaji ,miaka 30 kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha na miaka 3 kosa la uporaji wa simu hivyo kulazimika kutumikia miaka 63 kwa pamoja.


" Huyu mshitakiwa baada ya kusomewa hukumu alimweleza hakimu kuwa hawezi kabisa kutumikia miaka  63 aliyohukumiwa ......wakati akitolewa katika chumba cha mahakama kupelekwa mahabusu ya muda mahakamani hapo, kabla ya kwenda kuanza kutumikia adhabu yake alijaribu kutoroka kwa kujichanganya na wananchi waliofika mahakamani hapo na kutaka kukimbia kabla ya polisi kufyatua risasi hewani kwa ajili ya kumtaka ajisalimishe mwenyewe ila hakufanya hivyo na kutaka kuendelea kukimbia ",alieleza Kamanda.


Alisema kutokana na mfungwa huyo kuendelea kukimbia ndipo askari mmoja aliweza kuifanya kazi hiyo kwa umakini na kufanikiwa kumpiga risasi katika makalio na mguuni na kufanikiwa kumkamata na kumpeleka Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kwa matibabu .


" Ninampongeza sana askari aliyeanikisha kumkamata mfungwa huyo kwani bila umakini wa askari huyo polisi tungelaumiwa kuwa tumemtorosha mfungwa huyo aliyefungwa miaka 63 kwa ubakaji Raia wa kigeni waliofika mahakamani hapo walikuwa wengi sana kufuatilia mwenendo wa kesi hiyo "


Mganga wa mifupa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa Charles Lema alisema hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri na kuwa atakuwepo wodini kwa wiki zisizopungua 6 akipatiwa matibabu ya majeraha hayo kwani alisema alijeruhiwa paja la kushoto na mkono wa kulia.

Alisema hali ya mkono ni nzuri kwani hakuna mfupa ulioguswa na risasi hiyo ila mguu wake wa kushoto kuna mfupa ulipata majeraha na risasi moja ilimpata jirani na maeneo yake ya siri .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments