MWANAMME AHUKUMIWA KULIPA FAINI BAADA YA KUBOFYA 'LIKE' FACEBOOK

Kuna wasiwasi huenda hukumu hiyo ikatoa mfano mbaya wa kurejelewa kisheria Uswizi

Mahakama moja nchini Uswizi imempiga faini mwanamume mmoja aliyebofya alama ya kupenda au "like" kwa Kiingereza katika maoni yaliyotolewa kwenye ujumbe ulioandikwa katika Facebook.

Ujumbe huo ulikuwa wa kumharibia mtu mwingine sifa.

Kesi hiyo ilihusiana na maoni ambayo yalitolewa kumhusu Erwin Kessler, ambaye ni mkuu wa shirika la kutetea haki za wanyama.

Alidaiwa kuwa mweneza chuki dhidi ya Wayahudi na mbaguzi wa rangi, taarifa kwenye vyombo vya habari zinasema.

Mahakama ya ngazi ya wilaya mjini Zurich ilisema mshtakiwa "bila shaka alionekana kuunga mkono ujumbe huo na kuufanya kama wake" kwa kupenda maoni yaliyokuwa yametolewa.

Kwa mujibu wa gazeti la Le Temps la Uswizi, mwanamume huyo alibofya kitufe cha kupenda katika maoni sita.

Bw Kessler anadaiwa kuwashtaki watu zaidi ya kumi kuhusiana na maoni ambayo yalitolewa kwenye Facebook mwaka 2015.

Waliochangia wanatoa maoni kuhusu mjadala wa iwapo makundi ya kutetea haki za wanyama wanafaa kuruhusiwa kushiriki katika tamasha la wasiokula nyama, gazeti la Tages Anzeiger limeripoti.

Watu kadha wamepatikana na makosa, lakini hakuna aliyekuwa amepatikana na makosa awali kwa kupenda maoni yaliyotolewa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Bw Kessler aliwahi kuhukumiwa chini ya sheria za kukabiliana na ubaguzi wa rangi zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Mahakama iliamua kwamba mshtakiwa hangeweza kuthibitisha kwamba maoni aliyoyapenda yalikuwa ya kweli.

Mahakama hiyo ya Zurich ilisema kitendo cha "kupenda" maoni kinayafanya "kuonekana na watu wengi zaidi", na kwamba hatua hiyo iliathiri "heshima (kwa Kessler)".

Amepigwa faini ya faranka 4,000 za Uswizi (£3,200; $4,100) kwa mujibu wa AFP.

Ana haki ya kukata rufaa.

Wakili wa mmoja wa wengine walioshtakiwa na Bw Kessler amesema uamuzi huo wa mahakama unaweza kuwa na "madhara makubwa" licha ya kwamba ulifanywa na mahakama ya kanda.

Amr Abdelaziz amesema mahakama Uswizi zinahitaji kutoa ufafanuzi kwa watu wanaotumia mitandao ya kijamii na kuonga kwamba uhuru wa kujieleza huenda ukaathiriwa pakubwa iwapo watu watahukumiwa kwa "kupenda" ujumbe kwenye Facebook.
Via>>BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments